Kimataifa

Watu 12 wauawa katika shambulio la bomu kwa kambi za wakimbizi DRC

May 4th, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

GOMA, DRC

WATU 12, wakiwemo watoto, wameuawa katika milipuko ya mabomu iliyorushwa katika kambi mbili za watu waliopoteza makao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kulingana na maafisa wa serikali na Umoja wa Mataifa (UN).

Mashambulio hayo ya Ijumaa yalilenga kambi hizo zilizoko maeneo ya Vert na Mugunga karibu na Goma, jiji kuu la mkoa wa Kivu Kaskazini, UN ilisema kwenye taarifa.

“Mashambulio hayo yanakiuka sheria ya kimataifa kuhusu haki ya kibinadamu na yanayoweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita,” taarifa hiyo.

Zaidi ya watu 20 walijeruhiwa katika tukio hilo.

Mkazi mmoja katika mojawapo ya kambi hizo, aliwaambia wanahabari kwamba waathiriwa walikuwa wakilala katika mahema yao eneo hilo liliposhambuliwa.

“Tulianza kukimbia baada ya bomu kuanza kurushwa katika kambi,” mkazi mmoja alisema.

Jeshi la DRC na Amerika zilielekeza kidole cha lawama kwa wanajeshi wa Rwanda na wapiganaji wa kundi la waasi la M23 kwa kuhusika katika shambulio hilo.

Luteni-Kanali Guillaume Njike Kaiko, msemajhi wa jeshi la DRC eneo hilo, alisema mashambulio hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi mashambulio ya DRC katika vituo vya jeshi la Rwanda yaliyoharibu silaha zao.

Msemaji wa serikali Patrick Muyaya pia alielekeza lawama kwa M23 ambalo limechukuwa udhibiti wa sehemu kadhaa katika mkoa Kivu Kaskazini katika miaka miwili iliyopita.

Serikali ya DRC, UN na nchi za Magharibi zimedai kuwa Rwanda inasaidia kundi hilo la waasi kwa lengo la kudhibiti migodi na rasilimali ya madini mashariki wa nchi hiyo. Rwanda imekana tuhuma hizo.

Mnamo Ijumaa wanajeshi wanaotuhumiwa kuonyesha uoga na kukwepa majukumu yao wakikabiliana na M23 walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Goma.