Watu 12,000 wakwama penye vita Ukraine – UN

Watu 12,000 wakwama penye vita Ukraine – UN

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

MAELFU ya raia wamekwama katika mji wa Severodonetsk nchini Ukraine, Umoja wa Mataifa (UN) ukionya kuwa wengi wao hawana bidhaa za msingi za matumizi.

Hapo jana Alhamisi, UN ilisema kuwa wengi wanalazimika kulala kwenye mapango na mashimo yaliyo chini ya kiwanda cha kutengeneza kemikali cha Azot, mjini humo.

Daraja la mwisho ambalo wenyeji wa mji huo wangetumia kuondoka liliharibiwa wiki hii, hali ambayo imewafanya zaidi ya watu 12,000 kukwama.

Kwa majuma kadhaa, vikosi vya Urusi vimekuwa vikilenga kuuteka mji huo wote kutoka kwa udhibiti wa majeshi ya Ukraine.

Kwa sasa, Urusi ndiyo inadhibiti eneo kubwa la mji huo.

“Ukosefu wa maji na usafi ni hali inayotutia hofu sana. Tuna wasiwasi kwani watu hawawezi kuishi muda mrefu bila maji,” akaeleza Saviano Abreu, ambaye ndiye Msemaji wa UN kuhusu Masuala ya Kibinadamu.

Abreu aliongeza kuwa chakula cha msaada na dawa zilizotolewa kwa waathiriwa hao ziko karibu kuisha.

Mji huo uko katika eneo la Luhansk, mashariki mwa Ukraine.

UN ilisema kuwa inalenga kuwasaidia wale ambao wamekwama mjini humo, ijapokuwa mapigano yanayoendelea kati ya nchi hizo mbili yanaathiri utoaji misaada unaoendeshwa na mashirika yake.

Ulieleza kuwa wafanyakazi wa mashirika hayo hawawezi kuwafikia waathiriwa, ambapo wengi ni wanawake, watoto na wazee.

Onyo hilo linafuatia ahadi ya Urusi kubuni eneo maalum Jumatano, ambalo litatoa nafasi kwa watu waliokwama katika kiwanda hicho kupata usaidizi.

Kufikia sasa, hakuna thibitisho lolote kuhusu ikiwa Urusi imetimiza ahadi yake.

Jumatano, afisa mmoja wa serikali ya Ukraine anayeiunga mkono Urusi alivilaumu vikosi vya Ukraine dhidi ya kuwa “kikwazo” kwenye juhudi za kuwaokoa watu waliokwama katika kituo hicho.

“Katika kiwanda cha Azot, vikosi vya Ukraine vinajaribu kuvuruga juhudi za kuwaokoa watu waliokwama. Vimeanza kufyatua risasi na makombora kutoka kwa vifaru vyao,” akasema afisa huyo, Rodion Miroshnik.

Afisa huyo anatoka katika eneo moja la Luhansk, ambalo limetangaza kujitenga na Ukraine. Vyombo vya habari vya Urusi pia vilivilaumu vikosi vya Ukraine dhidi ya kuwatumia wenyeji kama “ngao”, hivyo kuvuruga juhudi za kuwaokoa waathiriwa.

Wakati huo huo, viongozi wa mataifa matatu barani Ulaya jana walifanya ziara maalum nchini Ukraine, kwenye harakati za kuonyesha uungwaji mkono wa bara hilo kwa Ukraine.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Chansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi, waliwasili jijini Kyiv jana asubuhi, baada ya kusafiri kwa gari la moshi kuanzia Jumatano.

Ziara hiyo ndiyo ya kwanza kufanywa na viongozi wakuu wa mataifa ya Ulaya kwa pamoja nchini humo.

Hakuna yeyote kati yao ambaye amezuru Ukraine tangu Urusi kuanza uvamizi dhidi ya nchi hiyo Februari.

Nchini mwao, Scholz na Macron wamekuwa wakilaumiwa kwa kutoizuru Ukraine.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine anatarajiwa kukutana na viongozi hao watatu ili kujadili jinsi Ulaya italisaidia taifa hilo kupata usaidizi wa silaha.

Watatu hao pia wanatarajiwa kujadili uwezekano wa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya (EU).

  • Tags

You can share this post!

KIPWANI: Kabisha majuzi tu tena kwa mshindo

Mong’are atolewa jasho na digrii yake

T L