Watu 13 waangamizwa na corona

Watu 13 waangamizwa na corona

Na CHARLES WASONGA

WATU 13 zaidi wamefariki kutokana na Covid-19 katika kipindi ambapo visa vipya 843 vya ugonjwa huo vimethibitishwa.

Kulingana na taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Waziri Mutahi Kagwe Jumapili, wagonjwa wawili walifariki ndani ya saa 24 zilizopita ilhali vifo 11 vilitokea awali katika hospitali mbalimbali wakati tofauti.

“Kwa hivyo, idadi jumla ya waliofariki kufikia Jumapili ni 2,117,” akasema Bw Kagwe.

Visa 843 vipya vya maambukizi viligunduliwa baada ya sampuli za watu 5,377 kupimwa; ishara kwamba kiwango cha maambukizi Jumapili kilikuwa asilimia 16, kulingana na Waziri Kagwe.

“Kwa hivyo, idadi jumla ya maambukizi nchini ni 130, 214 kutokana na jumla ya vipimo 1,468,835,” akaongeza.

Visa vipya vimeripotiwa katika kaunti mbalimbali kama ifuatavyo; Nairobi 509, Kiambu 99, Uasin Gishu 59, Machakos 48, Nakuru 46, Kajiado 38, Meru 13, Kitui 12, Nandi 11, Kilifi 9, Elgeyo Marakwet 5, Marsabit 5 na Bungoma 4.

Kaunti nyingine ni; Murang’a visa 3, Vihiga 3, huku kaunti za Kakamega, Laikipia, Nyandarua, Taita Taveta, Wajir, West Pokot, zikirekodi visa viwili kila moja. Nazo kaunti za Turkana, Baringo, Lamu, Migori, Mombasa, Garissa, Nyeri na Homa Bay zikinakili kisa kimoja kila moja.

Bw Kagwe pia amesema kuwa wagonjwa 89 walithibitishwa kupona ambapo 57 walikuwa wakiuguzwa nyumbani na 32 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali.

Kufikia Jumapili, jumla ya wagonjwa 1,221 walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali ilhali wengine 4,060 walikuwa wakiuguzwa nyumbani.

Jumla ya wagonjwa 121 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICUs), 32 wakiwa wamewekewa mitambo ya kuwaongeza oksijeni.

You can share this post!

Faida za lozi

ANC kusajili wanachama wapya