Kimataifa

Watu 18 wafa kwenye mgodi China

December 5th, 2020 1 min read

Na AFP

BEIJING, China

WACHIMBA migodi 18 Jumamosi, Desemba 5, 2020, walithibitishwa kufariki baada ya gesi ya ukaa kuvuja ndani ya mgodi wa makaa ya mawe kusini magharibi mwa China, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Shughuli za kuwaokoa wengine watano ambao walikuwa wamekwama kwenye mgodi huo zilianza mara moja.

Mkasa huo uliwakumba wachimba migodi 24 katika mgodi wa Diaoshuidong jijini Chongquig baada ya kuvuja kwa mtungi wa gesi hiyo ya sumu Ijumaa jioni, shirika la habari la kitaifa, CCTV, liliripoti.

Kufikia jana asubuhi, manusura mmoja na waathiriwa 18 walikuwa wamepatikana, ikasema CCTV, ikinukuu taarifa kutoka makao makuu ya shirika la uokoaji eneo hilo.

Kisa hicho kilitokea wakati wafanyakazi walikuwa wakifungua mitambo ya uchimbaji ndani ya mgodi huo ambao hapo awali ulikuwa umefungwa kwa muda wa miezi miwili.

Wapelelezi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali, shirika la habari la Xinhua lilisema.

Kisa cha hapo awali sawa na hicho, kilisababisha vifo vya watu watatu mnamo 2013, kulingana na Xinhua inayomilikiwa na serikali.