Habari Mseto

Watu 18 wakamatwa jijini Nairobi wakiwa uchi

April 27th, 2020 1 min read

HILLARY KIMUYU na VALENTINE OBARA

UOZO wa maadili miongoni mwa vijana unaendelea kuenea, wakati ambapo taifa linajikakamua kupambana na virusi vya corona.

Vijana wengi wanapuuza masharti yanayolenga kuepusha ueneaji wa virusi hivyo wanapotenda vitendo vya usherati, huku maelfu wengine wakikusanyika katika mitandao ya kijamii kwa minajili hiyo hiyo.

Jumatatu, polisi wameripoti waliwanasa watu 18 wenye umri wa kati ya miaka 14 na 30 katika mtaa wa Jamhuri jijini Nairobi mnamo Jumapili jioni wakiwa uchi wa mnyama.

Taarifa ya polisi wa kituo cha Kilimani imesema kwamba waliarifiwa na umma kuhusu tukio lisilo la kawaida.

Maafisa walipoenda, walikuta watu hao wa kiume na wa kike, wakiwemo wanne wenye umri chini ya miaka 18 wakitengeneza video.

Wiki iliyopita, vijana 21 walikamatwa katika Kaunti ya Nakuru wakipiga picha za uchi.

Naibu Kamishna wa Kaunti anayesimamia Nakuru Magharibi, Bw Elni Shafi, alisema vijana hao walinaswa baada ya wananchi kuarifu polisi.