Habari Mseto

Watu 3 waangamia ajalini Kitui

August 20th, 2020 1 min read

 KITAVI MUTUA na FAUSTINE NGILA

Watu watatu wameangamia kwenye ajali iliyotokea eneo la Kathivo karibu na soko la Kabati barabara ya Kanyonyonyoo –Thika Kaunti ya Kitui hapo Alhamisi.

Dereva wa matatu ya watu 14 ya Sacco ya Kimathi iliyokuwa ikielekea Nairobi alipoteza mwelekeo na kusabisha gari lake kubingiria mara kadhaa.

Mafisa wa polisi waliotembelea eneo la mkasa waliambia Taifa Leo kwamba dereva huyo aliamua kufuata makutano ya barabara hiyo baada ya kuyapita na kusababisha ajali.

“Barabara hii inajengwa na kuna uwezekano dereva alikuwa anaendesha gari kwa mwendo wa kasi alipogundua kwamba alikuwa agonge mchanga uliokuwa umefunga barabara,” alisema afisa wa polisi wa trafiki.

Mtoto mmoja alifariki papo hapo huku watu wengine wawili wakitangazwa kufariki baada ya kufikishwa hospitali ya Kitui.

Kulingana na Virginia Muviku, walipokea watu saba waliokuwa wameumia akiwemo dereva wa matau hio.

“Watano hao walikuwa na maumivu tofauti tofauti lakini tumefanikiwa kuwatuliza na wako sawa kwa sasa,”alisema Dkt Muviku.

Miili ya waliofariki ilipelekwa kwenye chumba cha maiti cha hospitali hiyo.