Habari Mseto

Watu 3 zaidi wameonyesha dalili za corona – Serikali

March 16th, 2020 1 min read

Na VALENTINE OBARA

Serikali imesema kuna watu watatu wanaoonyesha dalili za kuugua virusi vya corona, mbali na watatu waliothibitishwa kuugua kufikia Jumatatu.

Msemaji wa serikali, Bw Cyrus Oguna, amesema watatu hao ni miongoni mwa 22 ambao walikuwa wametangamana na mgonjwa wa kwanza aliyetangazwa Ijumaa.

Akihutubia wanahabari Nairobi, Bw Oguna alisema wengine wawili walithibitishwa hawana dalili zozote za corona wakaruhusiwa kwenda nyumbani.

Hivyo basi, wale ambao bado wamelazwa ni 20. Watatu wamethibitishwa kuambukizwa, watatu wameonyesha dalili, na 14 wangali wametengwa wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa kimatibabu.

“Watatu wanaoshukiwa kuambukizwa walionyesha dalili za virusi vya corona kama vile kukohoa, matatizo ya kupumua na joto jingi mwilini,” akasema.

Aliongeza kuwa serikali ingali inatafuta watu wengine waliotangamana na mgonjwa wa kwanza.

Kuhusu mgomo baridi wa wauguzi uliotokea asubuhi katika Hospitali ya Mbagathi, alisema walioshiriki mgomo huo si wanaohudumia vitengo vya corona lakini serikali ilitatua malalamishi yao.