Habari

Watu 3,000 wajitokeza kupimwa Covid-19 Nairobi

May 26th, 2020 1 min read

NA COLLINS OMULO

WATU 3,000 wamejitokeza kupimwa virusi vya corona jijini Nairobi Jumanne, katika zoezi linaloendeshwa na Idara ya Huduma za Nairobi.

Zoezi hilo la siku 11 lilianzishwa Jumatano wiki iliyopita na tayari watu 3,144 wameshapimwa katika  muda wa siku tano zilizopita.

Mkuu wa Idara hiyo Ouma Olunga alisema kwamba watu jijini Nairobi wamejitokeza kwa wingi na wanalenga kupima wakazi 1,000 kila siku.

Alisema kwamba watu 703 walipimwa mtaani Eastleigh Jumatano iliyopita huku wengine 427 wakipimwa Dagoretti na Embakasi Kaskazini.

Watu 1,002 walipimwa mtaani Utawala, Embakasi Kusini huku wengine 427 wakipimwa eneo la Embakasi Mashariki Jumapili, huku jumla ya watu waliopimwa Kaunti Ndogo ya Starehe ikifikia watu 585.

Dkt Oluga alisema kuwa upimaji huo unalenga kufahamu maeneo yalioathirika zaidi ili hatua za kiafya zichukuliwe.