Habari Mseto

Watu 32 waliotengwa kupimwa corona Mandera watoweka

April 14th, 2020 1 min read

Na MANASE OTSIALO

SERIKALI ya Kaunti ya Mandera, imejipata njiapanda baada ya watu 32 waliokuwa wametengwa kusubiri kuthibitishwa ikiwa wana virusi vya corona mjini Elwak kutoweka katika hali ya kutatanisha.

Serikali ya Kaunti haijui ikiwa watu hao waliachiliwa na maafisa wa usalama au walitoroka.

Lakini serikali ya kaunti kupitia barua yake kwa Kamishna wa Mandera Kusini (DCC) Abdihakim Dubat, inaonekana kushutumu maafisa wa serikali ya kitaifa kwa kuachilia huru watu hao bila kufuata utaratibu uliowekwa.

“Tunakuandikia barua kuelezea masikitiko yetu kuhusu kutoweka kwa abiria 32 kati ya 66 waliokuwa karantini mjini Elwak,” inasema barua hiyo iliyotiwa saini na afisa wa serikali ya Kaunti ya Mandera Ahmed Sheikh, ambaye anaongoza kamati ya kukabiliana na virusi vya corona katika eneo la Mandera Kusini.

“Inaonekana kwamba baadhi ya maafisa wa usalama hawaelewi uzito wa janga la virusi vya corona,” ikasema barua hiyo.

Serikali ya kaunti sasa inashutumu maafisa wa polisi kwa kuwatorosha abiria hao waliowekwa karantini kwa lazima baada ya kunaswa wakisafiri kutoka Nairobi kuelekea Mandera, Jumatano wiki iliyopita.

Walinaswa walipowasili mjini Elwak baada ya kufanikiwa kukwepa vikwazo vilivyowekwa barabarani na polisi. Walinaswa siku mbili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku watu kuondoka au kuingia jijini Nairobi.

Rais Kenyatta pia alipiga marufuku kutoka au kuingia katika Kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale.

Dereva wa gari hilo alikamatwa lakini jana hakufikishwa mahakamani kama ilivyotarajiwa.

Serikali ya Kaunti inataka Kamishna wa Mandera Kusini kuwasaka abiria hao na kisha awaadhibu maafisa wa polisi waliowaruhusu kuondoka.