Na MASHIRIKA
JUBA, SUDAN KUSINI
WATU 32 wameuawa, 17 wakajeruhiwa na nyumba kadhaa kuteketezwa katika shambulio lililotekelezwa Jumatatu jioni katika kaunti ya Bor, jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini, maafisa walisema Jumanne.
Kamishna wa kaunti hiyo, Yuot Alier alisema kisa hicho kilitokea kundi la vijana wenye silaha walipovamia eneo la Baidit Jumatano jioni.
“Watu hao 32, ni pamoja na wavulana wawili, msichana mmoja na wanawake wawili na wanaume kadha. Watoto wengi walikufa maji,” Kamishna Alier akasema.
“Kisa hicho kilitokea Jumatatu mwendo wa saa kumi na moja jioni. Nyumba tano ziliteketezwa na ng’ombe 2600 kuibiwa katika uvamizi huo,” akaongeza.
Alisema vijana wa eneo hilo wanasaka wavamizi hao.
“Vijana wetu wanawafuatilia wavamizi hao. Kwa hakika hao ni vijana wa Murle na wanatoka eneo la Pibor. Maafisa wa serikali eneo hilo wanafaa kuwajibikia kitendo hicho kwa sababu vijana hao sio wahalifu,” akaongeza.