Habari Mseto

Watu 4 waangamia kwenye ajali iliyohusisha basi la Climax

February 24th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WATU wanne walifariki Jumapili asubuhi kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la Morendat katika barabara ya Nairobi kwenda Nakuru.

Ajali hiyo ilitokea pale gari aina ya Toyota Wish ilipogongana na basi la kampuni ya uchukuzi wa abiria ya Climax.

Gari hilo lilikuwa likisafiri kwenda Nairobi lilipogongana ana kwa ana na basi hilo mwendo wa saa kumi na mbili alfajiri.

Waliofariki walikuwa wakisafiri katika gari hilo dogo huku abiria kadhaa waliokuwa ndani ya basi wakijeruhiwa. Majeruhi walikimbizwa katika katika hospitali ya Naivasha ambako wamekuwa wakipokea matibabu.

Kwingineko watu wanne walifariki katika ajali nyingine ya barabarani katika kaunti ya Bungoma

Watu hao walifariki pale gari la matatu la kubeba abiria 14 lilipogongana na lori katika kituo cha kibiashara cha Marakaru katika na Chwele.

Mbunge wa Kimilili ni miongoni mwa watu waliofika eneo la tukio saa chache baada ya ajali hiyo kutokea.

“Kati ya waliofariki ni rafiki yangu wa dhati ambaye pia ni diwani wa zamani wa Wundanyi,” Mbunge huyo akasema.

Hata hivyo, ripoti ambazo hazikuthibitishwa zilisema kuwa miongoni mwa waliofariki walikuwa ni watoto ambao walikuwa wakielekea nyumbani baada ya kurejea kutoka likizo fupi.