Watu 41 wauawa 29 wakijeruhiwa katika vita vya kikabila Sudan

Watu 41 wauawa 29 wakijeruhiwa katika vita vya kikabila Sudan

Na AFP

KHARTOUM, Sudan

WATU wasiopungua 41 waliuawa na wengine 29 kujeruhiwa kutokana na vita vya kikabila eneo la Mashariki mwa El-Geneina katika jimbo la Darfur Magharibi, nchini Sudan.

Licha ya utulivu eneo hilo, uhasama wa kikabila, ambao ulikuwa kiini mojawapo cha michafuko mnamo 2003 – umeendelea kuchukua mikondo mbalimbali.

Ghasia jimboni Darfur Magharibi zilichochewa na kifo cha mwanachama wa makundi ya Kiarabu kwenye eneo la El-Geneina kufuatia ugomvi karibu na kambi ya walemavu ya Crendingue kutoka jamii ya Masalit.

Asaad Bahr al-Din, kiongozi wa Masalit alisema idadi ya watu waliouawa kutoka kabila lake ilikuwa karibu watu 30 huku watu wapatao 14 wakijeruhiwa.

Hata hivyo, alisema idadi hiyo haikuwa kamili maadamu waliendelea kupokea ripoti kuhusu wahasiriwa.

Alieleza vyombo vya habari nchini humo mnamo Jumanne kwamba, baadhi ya miili ya watu waliokuwa katika kambi hiyo, ambayo idadi yake bado haijulikani, ingali humo na hakuna anayeweza kuingia kuichukua.

“Baadhi ya miili ingali haijazikwa na haijulikani ilipo kwa kuwa hakuna anayeweza kukaribia mahali ambapo miili hiyo ipo,” alisema.

Alieleza vilevile kuwa, mamia ya wakimbizi wa ndani kwa ndani viungani mwa El Geneina walikimbilia taifa jirani la Chad, wakihofia maisha yao huku maelfu wakikimbilia vijiji vya mashinani.

 

Tafsiri imefanywa na Mary Wangari

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Inawezekanaje mwalimu wa Kiswahili...

Askofu Ole Sapit awataka wanasiasa wapunguze joto la...

adminleo