Kimataifa

Watu 60 bado hawajulikani waliko Lebanon

August 8th, 2020 1 min read

Na AFP na FAUSTINE NGILA

BEIRUT, Lebanon

ZAIDI ya watu 60 bado hawajulikani waliko siku nne baada ya mkasa wa mlipuko uliotokea jijini Beirut na kupelelekea vifo vya zaidi ya watu 150, afisa wa wizara ya afya alisema Jumamosi.

“Idadi ya waliofariki ni 154, wakiwemo watu 25 ambao hawajatambuliwa,” afisa huyo akaambia AFP.

“Vile vile, zaidi ya watu 60 bado hawajulikani waliko.” Akasema.

Mnamo Ijumaa, waziri huyo wa afya alisema kuwa watu 120 kati ya watu 5,000 waliojeruhiwa katika mkasa huo wa Jumanne, wako katika hali mahututi.

Wakati huo huo, Rais wa Lebanon Michel Aoun amepinga wazo kwamba wapelelezi kutoka mataifa ya kigeni wachunguze mkasa huo akisema huenda ulisababishwa na kombora au mapuuza ya wafanyakazi.

Alisema hayo huku makundi ya waokoaji yakiendelea kuchakura mabaki ya majengo wakisaka manusura.

Viongozi nchini Lebanon wanaendelea kulaumiwa kutokana na mlipuko huo uliotokea Jumanne na ambao ulisababisha uharibifu mkubwa jijini Beirut.

Mnamo Ijumaa Rais Aoun aliungama kuwa mfumo wa utawala nchini humo unapasa kufanyiwa mabadiliko.