Watu 7.1 milioni wamepata chanjo dhidi ya corona kufikia sasa – Uhuru

Watu 7.1 milioni wamepata chanjo dhidi ya corona kufikia sasa – Uhuru

Na SAMMY WAWERU

WATU 7.1 milioni wamepata chanjo ya virusi vya corona nchini kufikia sasa, ametangaza Rais Uhuru Kenyatta.

Akihutubia taifa Jumanne kupitia kikao cha pamoja bungeni, Rais Kenyatta alielezea matumaini yake lengo la watu 10 milioni kupata chanjo ya Covid-19 kufikia Desemba mwaka huu huenda likatimia.

“Mwezi Juni niliahidi kufikia Desemba 2021, watu 10 milioni watakakuwa wamepata chanjo.

“Kutoka idadi ya watu 5 milioni wakati wa maadhimisho ya Mashujaa Dei (Oktoba 20), leo hii jumla ya 7.1 milioni wamepata chanjo. Hii ina maana kuwa shabaha ya 10 milioni tutaiwahi kufikia Desemba mwishoni mwa mwaka huu,” akasema Rais.

Kiongozi wa nchi kwenye hotuba yake alihimiza wale ambao hawajapata chanjo, kujitokeza kwa wingi “ili Kenya ishinde ugonjwa huu ambao ni janga la kimataifa”.

Akiomboleza walioangamizwa na corona tangu kisa cha kwanza kithibitishwe nchini Machi 2020, Rais Kenyatta alisema shime kuu kwao ni kila mmoja kuhakikisha amepata chanjo.

“Tuwakumbuke na kuwavulia kofia ya shime kwa kila mmoja kupata chanjo ili kuzuia maafa zaidi,” akahimiza.

Serikali imekuwa ikitoa chanjo ya corona, kuanzia Machi 2021 na ambayo haitozwi malipo.

Aidha, chanjo zinazotolewa nchini ni Pfizer, Johnson & Johnson, Moderna na AstraZeneca.

Zinatolewa katika vituo vya afya vya umma, na vya kibinafsi vilivyopewa kibali, pamoja na hospitali, kwa njia ya kudungwa sindano.

Ili kupata, unahitaji kujisajili kupitia tovuti maalum ya Wizara ya Afya inayofahamika kama Chanjo Kenya (https://portal.health.go.ke/) ambapo unapaswa kufungua akaunti, ujaze maelezo binafsi kwenye fomu mtandaoni.

Takwimu

Rais alisema kufuatia mikakati ya serikali kupambana na corona, kwa siku watu 100,000 wanapata chanjo.

“Kwa muda wa siku 25 zijazo, ninawahimiza wale ambao hawajapata chanjo tujitume,” akasema.

Kwa mataifa ambayo yanatishia kutoa ilani ya kusafiri nchini mwao kutokana na mchipuko wa aina mpya na hatari ya corona Afrika Kusini, Rais aliyataka yafahamu kwamba Kenya ni makini katika vita dhidi ya corona.

Kirusi cha Omicron, kulingana na Shirika la Afya Duniani – WHO kinasambaa kwa kasi.

“Hatutashinda Covid kwa kutuwekea vikwazo… Hakuna ambaye atakuwa salama hadi sote tutakapokuwa salama. Jamani msitufungie, tumefanya kazi,” Rais Kenyatta akasema.

You can share this post!

Mafuriko yashuhudiwa mjini Thika

Otieno achanja pasi muhimu AIK ikizoa ushindi muhimu Ligi...

T L