Habari Mseto

Watu 7 wauawa katika vita vya Wajir-Marsabit

June 12th, 2020 1 min read

NA BRUHAN MAKONG

Angalau watu saba wamefariki kutokana na vita vya kijamii kati ya jamii zinazoishi mpakani wa Wajir na Marsabit vilivyoanza siku chache zilizopita.

Hofu imeshamiri eneo hilo walioathirika wakikimbilia usalama wao katika kaunti ndogo jirani ya Basir.

Familia zaidi ya 150 zimeathiriwa na na mapigano hayo huku Naibu Gavana wa kaunti ya Wajir Ahmed Mutar, kikosi cha usalama cha kaunti hiyo na maafisa wa Msalaba Mwekundu wakitembelea eneo hilo Jumatano.

Walichanga fedha za chakula na vifaa muhimu kwa watu waliopoteza makao.

Kulingana na Bw Muktar watu saba tayari walikuwa wamezikwa kufikia Jumatano lakini wawili bado walikuwa hawajazikwa.

Kamishna wa kaunti ya Wajir Jacob Narengo aliwaomba wanajamii wakae kwa amani huku serikali ikitafuta suluhu ya tatizo hilo

.“Tuko hapa kuomboleza na familia kufuatia vita hivyo. Tunajua kwamba watu saba tayari wamezikwa na wengine bado hawajapatikana na wawili bado hawajazikwa,” alisema Bw Muktar.