Makala

Watu 8 wakamatwa wakiuziwa pombe ndani ya choo Murang’a

April 7th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI 

WATU wanane waliokuwa wakisherehekea pombe wakiwa kwenye choo katika Mji wa Kenol, Murang’a kabla ya saa za baa kufunguliwa wametiwa mbaroni.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini, Bw Gitonga Murungi, msako mkali unaoendelezwa dhidi ya wakiukaji wa sheria ndio uliozua ubunifu huo.

Shida ilitokea wakati ambapo washukiwa hao walilemewa na makali ya mvinyo, wakaanza kuimba.

Aidha, inasemekana majirani waliposkia waliarifu maafisa wa polisi ambao walichukua hatua.

“Mmiliki na wahudumu wa baa husika walibuni ujeuri wa wateja kufungiwa kwenye choo na kisha wanauziwa pombe kabla ya saa rasmi kufika,” akasema Bw Murungi.

Afisa huyo alisema kwamba dokezi za majirani kwa maafisa wa usalama ziliishia uvamizi na ndipo washukiwa hao wakanaswa.

“Tulifika mahali hapo kwa awamu na tukawafumania wahudumu wakiwapitishia pombe kwa choo. Tulifanikiwa kunasa wanawake wawili na wanaume sita,” akasema.

Bw Murungi alisema kwamba wote watafikishwa mahakamani Jumatatu, Aprili 8, 2024 wakikabiliwa na mashtaka ya kukiuka sheria za uratibu wa biashara ya vileo.

Alisema kwamba “kuna hata uwezekano wa baa hiyo kupokonywa leseni yake kwa kuwa ukiona mhudumu ambaye anakaidi wito wa Rais William Ruto na Naibu wake, Rigathi Gachagua ambao ndio wanaendeleza vita hivi, ina maana hakuna afisi nyingine wanaweza wakaheshimu”.

Alisema kwamba baa hiyo imewekwa katika ploti ambayo imejaa wapangaji walio na watoto kinyume na masharti ya biashara ya vileo.

“Baa hiyo iko katika ghorofa la kwanza katika ploti ambayo imejaa wapangaji. Ukitoka kwa milango ya wapangaji unakumbana na walevi. Leseni ya baa hiyo ni haramu,” akasema.

Bw Murungi alionya kwamba hakuna baa itakubaliwa kuuza pombe kabla ya saa 11 jioni na baada ya saa tano usiku.

Hayo yamejiri huku naye Gavana wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata akitangaza kwamba baa zitaanza kupigwa msasa kuanzia Aprili 10 hadi Aprili 12, 2024 ili leseni zitolewe upya.