Habari Mseto

Watu 8 washtakiwa kunyang'anya Muriuki Sh100,000

May 21st, 2018 1 min read

Mshukiwa wa nane, Hussein Suleiman ashtakiwa kwa kumnyang’anya kimabavu Timothy Muriuki pesa katika hoteli ya Boulevard. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

SHAMBULIZI la mfanyabiashara Timothy Muriuki limepelekea washukiwa wanane kushtakiwa kwa kumnyang’anya Sh100,000..

Mnamo Alhamisi  Bw Hussein Suleiman alifikishwa kortini kuhusiana na shambulizi hilo.

Alikabiliwa na shtaka la kumnyang’anya Bw Muriuki katika hoteli ya Boulevard Nairobi na kumwumiza wakati wa kitendo hicho.

Katika picha zilizopigwa kuhusu shambulizi hilo Bw Suleiman alionekana akimnyanyua mlalamishi na kumfurusha nje ya hoteli hiyo.

Bw Suleiman alishtakiwa hwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Alikanusha shtaka la kumnyang’anya kimabavu Bw Muriuki pesa na wakati wa kitendo hicho wakamuumiza.

Kiongozi wa mashtaka Bi Pamela Avedi hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

“Kuna kesi nyingine tatu zilizofikishwa kortini kuhusu shambulizi hili la Bw Muriuki. Tayari washukiwa wengine saba wameshtakiwa. Kesi hii itaunganishwa na hizo nyingine tatu,” alisema Bi Avendi.

Bi Avedi aliambia mahakama kuwa katika kesi hizo nyingine washukiwa waliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema kesi hiyo itaunganishwa mnamo Mei 23, 2018.

Wakili Cliff Ombeta anayemtetea mshtakiwa aliomba korti baada ya kesi kuunganishwa upande wa mashtaka uagizwe umkabidhi nakala za mashahidi.

Bi Mutuku aliamuru Bw Suleiman aachiliwe kwa dhamana ya Sh200,000 sawa na washukiwa wale wengine walioshtakiwa awali. Aliamuru kesi dhidi ya Bw Suleiman iuanganishwe na zile nyingine.

Korti iliorodhesha kesi kusikizwa Julai 17.

Video Gallery