Habari Mseto

Watu 9 waangamia ajalini eneo la Kimende

August 29th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

ANGALAU watu tisa waliaga dunia Jumanne usiku baada ya ajali mbaya kutokea kati ya matatu na lori, katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru, katika eneo la Kimende.

Kulingana na walioshuhudia pamoja na ripoti za polisi, ajali hiyo ilitendeka saa tano usiku wakati matatu hiyo ya wateja 18 ilipogongana ana kwa ana na lori lililokuwa likielekea Nairobi.

Watu tisa waliripotiwa kufa papo hapo, huku watatu wakidhibitishwa kufa walipofikishwa hospitali ya kimishenari ya Kijabe.

Miili ya waliokufa ilipelekwa chumba cha kuhifadhi maiti ya hospitali hiyo, huku uchunguzi kuhusu kiini cha ajali hiyo ukianzishwa.

Walioshuhudia walisema wakati wa ajali kulikuwa na ukungu, ambao walidhani huenda ulichangia pakubwa.
Mkuu wa trafiki eneo la Lari Ahmed Mohammed alisema gari hilo la abiria lilikuwa likielekea magharibi mwa nchi kutoka Nairobi.