Habari za Kitaifa

Watu kumwaga unga Afisi za Rachel Ruto na Dorcas Gachagua zikifutiliwa mbali


WAHUDUMU kadhaa katika Afisi za Mama wa Taifa Rachel Ruto na ile Mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi huenda wakajipata bila ajira kuanzia Julai 1, 2024 huku mipango inayoendeshwa chini ya usimamizi wa wawili ikitarajiwa kukwama.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kutangaza kuwa afisi hizo mbili hazitafadhiliwa kwa pesa za umma katika mwaka wa kifedha 2024/2025 unaoanza Julai 1.

Dkt Ruto, ambaye alikuwa akihojiwa na wahariri kutoka mashirika makuu ya habari nchini Jumapili usiku, Juni 30, 2024  katika Ikulu ya Nairobi, alisema amechukua hatua hiyo ili kutimiza sehemu ya matakwa ya vijana wa kizazi cha Gen-Z.

“Afisi kama hizi zimekuwepo hapo zamani lakini kuanzia mwaka ujao wa kifedha unaoanza kesho Julai 1, 2024 hazitatengewa fedha zozote kwa sababu hazitakuwepo. Aidha, tutaondoa afisi zingine ili tuweze kupunguza gharama ya serikali jinsi vijana wetu walivyopendekeza,” Rais Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa alieleza kuwa Afisi kama vile za Mawaziri Wasaidizi (CASs) na washauri wa viongozi mbalimbali wa serikali kuhusu masuala kadhaa ya uongozi, zitafutiliwa mbali kwa muda hadi pale uchumi utakapoimarika.

“Ingawa bunge liliidhinisha kwamba CASs wateuliwe, sitafanya hivyo hadi uchumi utakapoimarika. Tunalenga kupunguza gharama ya ulipaji mishahara katika sekta ya umma hadi kufikia kiwango kisichozidi asilimia 35 ya mapato ya serikali kila mwaka,” akaeleza.

Bi Ruto na Pasta Dorcas 

Katika makadirio ya bajeti yaliyosomwa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u Bungeni mnamo Juni 13, 2024, Afisi ya Bi Ruto na Afisi ya Bi Rigathi zilitengewa jumla ya Sh1.2 bilioni kufadhili shughuli yazo kuanzia Julai 1, 2024 hadi Juni 30, 2025.

Kwa mujibu wa mgao huo, Afisi ya Bi Ruto ingepata Sh696.6 milioni huku ile ya Bi Rigathi ikipata Sh557.5 milioni.

Tangu Septemba 13, 2022, Rais Ruto alipoingia mamlakani, Afisi ya Mama wa Taifa imekuwa ikiendesha shughuli za kidini na mipango ya kuwawezesha akina mama kujisimamia.

Aidha, afisi hiyo imekuwa ikiendesha mipango ya ukuzaji wa misitu kupitia upanzi wa miche ya miti.

Mwaka jana, 2023, Afisi ya Bi Ruto ilizindua mpango mahususi wa utunzaji msitu wa Kakamega, ambao unasemekana kuwa katika hatari ya kuangamizwa na wakataji miti kiholela.

Kwa upande mwingine, Afisi ya Bi Rigathi, ambaye ni mke wa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, imekuwa ikiendesha mipango ya kuwezesha mtoto mvulana.

Mipango ya Pasta Dorcas haswa inalenga vijana ambao wamekolea uraibu wa matumizi ya pombe na dawa za kulevya.

Kufutiliwa mbali kwa afisi hizo, bila shaka kutakwamisha mipango kama hii ambayo ilikuwa ikiendeshwa na kundi la wafanyakazi ambao sasa watajipata bila ajira.

Shinikizo la Gen Z

Juzi, Mbunge Maalum John Mbadi aliunga mkono pendekezo la Gen-Z’s kwamba afisi hizo zinafaa kufutiliwa mbali kwani zinatumiwa kufyonza fedha za umma bila sababu; pesa ambazo zingeelekezwa katika miradi na mipango yenye manufaa kwa wananchi.

“Sioni haja ya serikali kutenga mabilioni ya pesa kwa Afisi wa Mke wa Rais na Mke wa Naibu Rais ili wazunguke kote nchini kuendesha shughuli za maombi. Tuna mapasta na wainjilisti wa kutosha nchini,” Bw Mbadi akasema Jumanne, Juni 25, 2024 kwenye mahojiano katika Runinga ya Citizen.

Jumapili, Juni 30, Rais Ruto hakurejelea moja kwa moja Afisi ya Mkewe Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Bi Tessie Mudavadi, licha ya kwamba afisi hiyo pia huendeshwa kwa pesa za umma.

Hata hivyo, haijabainika ni mipango au miradi ipi Bi Mudavadi huendesha.