Habari

Watu mashuhuri walioangamizwa na kansa

July 30th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KIFO cha Gavana wa Bomet Joyce Cherono Laboso kimeongeza idadi ya watu mashuhuri ambao wameuawa na kansa nchini.

Laboso alifariki Wakenya wakiendelea kumuomboleza mbunge wa Kibra Ken Okoth aliyeaga dunia Ijumaa baada ya kuugua kansa ya utumbo.

Miongoni mwa watu maarufu ambao wamekufa kutokana na saratani ni aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom Bob Collymore aliyekufa mapema Julai.

Aliyekuwa mtangazaji wa runinga ya NTV Janet Kanini alifariki Machi 2017 baada ya kupigana na maradhi hayo kwa miaka miwili.

Aliyekuwa mtangazaji wa runinga ya NTV, Janet Kanini aliyefariki Aprili 1, 2017. Picha/ Maktaba

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nyeri Nderitu Gachagua alifariki Februari 2017 akiwa na umri wa miaka 64 baada ya kutibiwa kansa jijini London, Uingereza kwa miaka miwili.

Mwaka huo, aliyekuwa mbunge wa Kitui Magharibi Francis Nyenze alifariki baada ya kutibiwa saratai ya utumbo kwa miaka kumi. Alikumbana na mauti akiwa na umri wa miaka 60.

Aliyekuwa Mbunge wa Kitui Magharibi, Francis Nyenze aliyefariki mwaka 2017. Picha/ Maktaba

Aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Harvard, Profesa Calestous Juma, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 64 baada ya kuugua kansa pia.

Aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Harvard, marehemu Profesa Calestous Juma. Picha/ Maktaba

Mhadhiri huyo alikuwa akitibiwa katika hospitali moja jijini Boston, Amerika.

Mwaka 2018 aliyekuwa Seneta wa Kaunti ya Migori Ben Oluoch aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 55 baada ya kuugua saratani ya koo naye aliyekuwa mwenyekiti wa chama chama cha maendeleo ya wanawake Jane Kiano alifariki kutokana na kansa ya koo.

Jane, uhai wake ulizima kama mshumaa akiwa na umri wa miaka 74.

Mnamo Aprili 2018 aliyekuwa mbunge wa Baringo Kusini Grace Kipchoim alifariki akiwa na umri wa miaka 49 baada ya kuugua saratani ya utumbo wa muda mrefu.

Wengine ni aliyekuwa gavana wa Nyeri Nderitu Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Fedha, David Mwiraria.

Wakenya wanataka serikali kutangaza ugonjwa huo kuwa janga la kitaifa na kuweka mikakati kuhakikisha kuwa unagunduliwa mapema ili watu waweze kuwa na nafasi ya kupata matibabu.

Hii ni baada ya kuibuka kuwa ukigunduliwa mapema ugonjwa huo unaweza kutibiwa lakini ukigunduliwa ukiwa umeenea mwilini na kukomaa huwa ni vigumu kutibiwa.

Kulingana na Gavana wa Kisumu Profesa Peter Anyang Nyongo ambaye alitibiwa saratani ya kibofu akapona, ugonjwa huo unapona iwapo utagunduliwa na kushughulikiwa mapema.

Dkt Andrew Odhiambo, mtaalamu wa maradhi ya saratani anasema kutogunduliwa mapema au kutibiwa maradhi tofauti kunasababisha vifo.

Hata hivyo anaeleza kuwa gharama ya kupimwa na kutibiwa saratani hutegemea na aina inayompata mtu.

Gharama ya matibabu ya saratani ni ya juu na huwa inalemea masikini na wanaharakati wa sekta ya afya wanasema watu wengi wamekuwa wakifariki.

Hii inathibitishwa na takwimu za wizara ya afya na shirika la Afya ulimwenguni zinazoonyesha kuwa watu 47 887 walipata kansa nchini Kenya 2018 na miongoni mwao 32,987 walifariki.

Kulingana na wataalamu wa saratani, inagharimu kati ya Sh172,000 na Sh759,000 kutibu saratani ya sehemu ya uzazi nchini na kati ya Sh672,000 na Sh1.25 milioni ikiwa mgonjwa atafanyiwa upasuaji.

Kutibu saratani ya matiti kunagharimu kati ya Sh175,000 hadi Sh1.98 milioni na gharama hii inaweza kuongezeka hadi Sh2.8 milioni kwa kutegemea hali ya matibabu anayohitaji mgonjwa