Makala

WATU NA KAZI ZAO: Mwanamke stadi katika uchomeleaji wa vyuma

November 19th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NI nadra kupata mwanamke anayefanya kazi ya uchomeleaji wa vyuma, maarufu kama welding kwa kuwa katika jamii ya mfumodume, inachukuliwa kazi ya jinsia ya kiume.

Inahusisha uunganisha wa vyuma, mabati kwa kutumia nguvu za umeme, kupitia vifaa maalum vinavyojulikana kama welding rodes.

Ukataji, ulainishaji na unowaji wa vyuma au mabati, hutekelezwa grainda. Kuna vifaa au vyombo vya kupima kama vile utepe.

Kimsingi, ni kazi ya mikono, inayodhaniwa wanaume ndiyo wanaiweza kwa sababu ya uhalisia wake. Kwa Mary Busuru, hilo kwake si hoja, anaamini kazi ni kazi na mchagua jembe si mkulima.

Licha ya kula chumvi, ni mchomeleaji vyuma wa aina yake. Hutengeneza vifaa kama mageti ya vyuma, milango, madirisha na vifaa vyovyote vile vya vyuma. Bi Mary Busuru, pia huchomelea magari na pikipiki.

Eneo la Mumbi, pembezoni mwa barabara inayounganisha mtaa wa Mwihoko na Githurai, tunampata Mary katika karakana yake. Amevalia vazi maalum, koti la samati iliyoshika, na anakamata chuma kinachopaswa kuunganishwa na mlango unaoendelea kutengenezwa.

Bi Mary Busuru, akikagua kimo cha chuma chembamba kuchomelea kwenye mlango. Picha/ Sammy Waweru

“Hapa ni kazi tu, pamoja na wafanyakazi wangu. Chuma hiki chembamba ni cha kuunganisha na huu mlango, katika harakati za kukamilisha uundaji wake,” akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano. Mary ana mafundi watatu.

Aliingilia kazi hiyo ipatayo miaka kumi iliyopita, na anasema ni gange ya mikono, macho, na akili.

Kulingana naye, hakujiunga na chuo chochote kile cha mafunzo ya vyuma na uhunzi. Alikuwa mfanyabiashara, na ni katika ziara yake mtaa wa Kariobangi alikutana na mzee mmoja anayefanya kazi hiyo, akafurahishwa nayo.

“Nilimtembelea mara kadhaa, akanipa mwaliko wa kujifunza. Ilinichukua takriban miezi sita kufahamu bayana uchomeleaji wa vyuma,” anadokeza.

Baada ya kujihami na ujuzi na maarifa faafu, Bi Mary Busuru ambaye ni mama wa watoto wanne, alijitosa uwanjani.

“Utangulizi haukuwa rahisi. Nilikuwa nikipokea oda za kutengeneza milango na mageti, na licha ya kufanya makosa, mengine yaliyofanya nikadirie hasara niliendelea kujiimarisha,” afafanua. Muhimu katika kazi ya uchomeleaji vyuma, ni kuafikia matakwa ya wateja, ambao walimkosoa na ni kupitia hilo ameweza kujiimarisha.

Oda nyingi anazopokea ni za milango na mageti. Vigezo muhimu kuzingatia ni vipimo na muundo wa vifaa anavyotakiwa kutengeneza.

Mary ana wafanyakazi watatu, ambao amewafunza na kuwanoa gange hiyo. “Karakana hii ndiyo ofisi yetu. Mama ndiye mwelekezi na mtaalamu wetu,” anasema mfanyakazi mmoja. Kwa kuwa miaka inazidi kusonga, Mary sasa anafanya kazi ya usimamizi na kuwaelekeza.

Wakati wa uchomeleaji, anayefanya shughuli hiyo anapaswa kuvalia miwani spesheli ili kuzuia vyuma vidogovidogo kuingia machoni.

“Ni muhimu pia kuwa aproni kwa sababu ya cheche za moto zinazotolewa na rodes (nyaya za kuunganisha),” anaelezea.

Katika kazi ya uchomeleaji vyuma, mteja hujinunulia vyuma vya vifaa anavyoundiwa, chuma na nyaya za kuunganisha.

“Humfanyia bajeti, kisha sisi tunatoza ada ya leba kulingana na uhalisia wa kazi,” anasema Mary.

Kwa hakika, ni kazi ya sanaa asiyojutia kamwe na yenye mapato akilinganisha na aliyokuwa akifanya awali.

Katika simulizi yake, mama huyo hakosi wosia kwa wanawake wenza akiwapa motisha kujitosa katika gange ya aina hiyo. Anasema nyakati za ubaguzi wa kazi kwa msingi wa jinsia ya kike na kiume zilipitwa, na kwamba gange zinazofikiriwa ni za kike pekee wanaume wanazifanya na hata kubobea zaidi, sawa na zinazodhaniwa ni za kiume.

“Siku hizi tunaona wanaume wakifanya ususi na usongaji wa nywele, kazi yenye dhana kuwa ni ya wanawake. Wanawake wajitokeze na kufanya kazi zinazofikiriwa ni za wanaume, hakuna kisichowezekana. Kujitolea na mapenzi kwa kazi, ndicho kiini cha ufanisi,” anashauri mama huyo.