Makala

WATU NA KAZI ZAO: Ukakamavu umemwezesha kujiimarisha licha ya changamoto

November 12th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BI Irene Maina amesomea upishi, na ni taaluma aliyoienzi tangu akiwa na umri mdogo.

Alifanikiwa kupata nafasi ya ajira Maralal, Kaunti ya Samburu.

Hata hivyo, baada ya kuifanya kwa miaka kadha aliipoteza mwaka 2012 na ni wakati anaosema aliihitaji kwa hali na mali.

“Nilikuwa nimejaaliwa mtoto akiwa na umri wa miaka miwili wakati huo,” anasema Irene.

Anasimulia kwamba hakuwa na budi ila kuungana na jamaa zake jijini Nairobi, ili kumsitiri pamoja na malaika wake.

Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki.

Irene anasema dada yake mzawa alimpokea, ingawa hakuhisi kutaka kuwa ‘mzigo’ kwake kwani pia alikuwa na familia yake. Isitoshe, chochote alichomiliki Maralal alikiacha kwa sababu ingekuwa ghali kusafirisha.

Aliyetarajia kufunga naye pingu za maisha, alisalia kimya wakati akipitia changamoto zote hizo. Hiyo ni licha ya kuwa nguzo yake kuu, hususan kumpiga jeki katika biashara.

“Hakuna jambo gumu maishani kama kujisimamia halafu unafilisika ghafla,” anasisitiza mama huyo wa mtoto mmoja.

Kwa kuwa alipokuwa kazini alikuwa mtu wa watu, na aliwatendea wema, dada yake hakuona ugumu wowote kumfaa.

Kulingana na Irene, alipata kazi ya uuzaji wa bima katika kampuni moja ya bima jijini Nairobi na ndipo alihamia eneo la Thika. Anasimulia kwamba dadake alimsaidia katika harakati hizo, na hata kugharamia kodi ya nyumba na mahitaji mengine.

Gange hiyo haikuwa rahisi kama alivyodhania, kwani ilikuwa na changamoto zake. Cha kusikitisha aliiraukia asubuhi na mapema, ikizingatiwa kwamba sharti angeandaa mwanawe na kumpeleka shuleni.

“Jioni mkondo ulikuwa ule ule wa marathon, kuendea mtoto shuleni, kumfulia sare na mavazi yake ya nyumbani na kumpikia. Keshoye pia nilitarajiwa ofisini. Ilikuwa kazi ya machovu,” anafafanua.

Mwanawe alikuwa angali mdogo, na wataalamu wa masuala ya watoto, wanasema mama ambaye ni mzazi wa karibu anapaswa kuwa sako kwa bako na mtoto kwa muda hadi atakapokomaa.

“Watoto pia hukumbwa na mawazo hasa wanapokosa uwepo wa mama. Lugha na malezi ya mama hayaambatani na ya yaya au mlezi tofauti. Kuna yale mapenzi ya mama kwa mtoto, yanayomfanya kukua kimawazo,” anaeleza Bi Karungari Mwangi, muuguzi mstaafu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya watoto, wakiwamo ambao hawajafikisha umri wa kuzaliwa (pre-term babies) pamoja na masuala ya lishe.

Kwa mujibu wa maelezo ya mdau huyo, ni muhimu mama hata akiwa kazini kupata muda wa kutosha haswa jioni na likizo kutangamana na kucheza na mwanawe, akiwa angali mchanga.

“Muda anaotangamana naye ni muhimu katika malezi na ukuaji wa mtoto,” anahimiza.

Ni kufuatia ushauri unaowiana na huo Irene Maina alikata kauli kuacha kazi hiyo na kuwekeza katika biashara 2017.

“Biashara yenyewe ilinoga hadi mwanzoni mwa mwaka huu, 2019, nikaamua kuifunga kwa sababu nilianza kukadiria hasara,” anasema.

Mama huyu anasema pandashuka alizopitia awali zilimfanya kuwa mkakamavu, na kumtegemea Mungu kwa kila jambo. Licha ya kufunga biashara asijue atakachofanya kukimu mwanawe, Irene anasema alijaaliwa kupata kandarasi ya usafirishaji wa mawe ya ujenzi, gange anayoifanya kufikia sasa.

Hali kadhalika, amefufua taaluma yake ya upishi anayosema imenoga.

“Ninafanya mapishi ya nje (outside catering). Hasa tunapokaribisha msimu wa Krismasi, ninapata oda chungu nzima za kupika katika harusi,” aeleza.

Anaambia Taifa Leo kwamba anapania kufungua biashara yake ya chakula na mengineyo yanayohusu upishi, ambapo kwa sasa anashughulikia vifaa vya mapishi kama vile majiko, sufuria na vihifadhio vya chakula.

Mwanauchumi na mhasibu Charles Mwangi, anasema hilo ataliafikia upesi ikiwa amekuwa akiweka akiba.

“Ni muhimu unapofanya kazi ujifinze kufunga mshipi wa tumbo, ukilipwa mshahara wa Sh20, weka akiba ya Sh5. Haijalishi kidogo unachoweka kando, kitakufaa kuafikia malengo yako maishani,” anashauri Bw Mwangi.