Habari Mseto

Watu sita waangamia, saba wakipata majeraha katika ajali ya magari ya kibinafsi Narok

April 22nd, 2024 1 min read

VITALIS KIMUTAI NA LABAAN SHABAAN

WATU 6 wamefariki na wengine 7 kujeruhiwa katika ajali ya barabara Narok Jumapili usiku.

Hii ni baada ya magari mawili ya kibinafsi kugongana ana kwa ana eneo la Silanga mwendo wa saa tatu na nusu.

Gari aina ya Toyota Sienta lilikuwa linatoka Narok kuelekea Mulot huku lile la Subaru Forester likisafiri kuingia Narok ajali ilipotokea.

Ajali hii imethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Narok ya Kati Joseph Momanyi.

“Jumla ya watu 13 walihusika katika ajali wakiwemo watoto 2. Waliojeruhiwa wanatibiwa katika hospitali mbalimbali,” Bw Momanyi alieleza.

Mili ya waliofariki inahifadhiwa katika makafani ya Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok.

“Abiria 5 na dereva wa Toyota Sienta walikata roho papo hapo huku manusura wakisafirishwa hospitalini wakiwa na majeraha,”  Bw Momanyi alifafanua.

Kamanda huyu wa polisi aliwaonya madereva dhidi ya mwendo wa kasi na kubeba mizigo kupita kiasi.

Bw George Nkurumwa, mwathiriwa wa ajali aliyesafiri kwa Sienta, alisema walikuwa 10 garini wakati wa tukio.

“Niliabiri gari mjini nikielekea nyumbani Katagala katika barabara kuu ya Ololunga-Narok lakini safari yetu ilikatizwa ghafla. Nilisikia kishindo kikubwa, kisha giza! Nilichojua baadaye ni kuwa nilikuwa juu ya kitanda cha hospitali,” Bw Nkurumwa alisema akiwa Hospitali ya Cottage, Narok.

Walioponea walisimulia kuwa walipelekwa kwanza katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Narok lakini hawakutibiwa kwa sababu ya mgomo wa madaktari unaoendelea.

Manusura mwengine, Bw Chris Saoli, alishuhudia kuwa gari aina ya Subaru lilikuwa linajaribu kupita gari jingine kabla ya kugongana na gari walilosafiria.

“Sikumbuki nini kingine kilifanyika kwa sababu tulijikuta hospitalini,” Bw Saoli alisema.