Habari Mseto

Watu tisa waaga dunia basi likianguka mtoni Mbagathi

May 18th, 2024 1 min read

NA MWANDISHI WETU

WATU tisa wamepoteza maisha Jumamosi asubuhi baada ya basi kuanguka katika Mto Mbagathi.

Ripoti ya polisi katika kituo cha polisi cha Ongata Rongai ilisema dereva wa basi la sacco ya Naboka, ambalo lilikuwa likitoka eneo la Gataka kuelekea upande wa Karen jijini Nairobi, alipoteza udhibiti na likatumbukia mtoni.

“Ajali ilitokea dakika 20 kabla ya saa nne asubuhi na watu sita waliaga dunia papo hapo huku wawili wakipoteza maisha walipokuwa wakipelekwa hospitalini. Wengine 18 walijeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali mbalimbali za karibu huku shughuli ya kuopoa basi ikiendelea,” ikasema ripoti ya polisi.

Iliongeza kwamba mtu mwingine alipoteza maisha na kufikisha idadi ya walioaga dunia kufikia tisa na majeruhi 17. Hilo pia lilithibitishwa na Naibu Inspekta Jenerali Mary Omari.

Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali za Karen, St Mary’s na Ngong.