Habari za Kaunti

Watu tisa waaga dunia kwenye ajali Nakuru

June 8th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

WATU tisa wameaga dunia Jumamosi katika Kaunti ya Nakuru kufuatia ajali iliyohusisha magari manne katika barabara ya Mai Mahiu-Nairobi.

Kulingana na ripoti rasmi ya polisi, watu wengine wanane wamejeruhiwa na wanapokea matibabu hospitalini.

“Mwendo wa saa sita hivi za mchana katika eneo la VIP kwa barabara ya Mai Mahiu-Nairobi, dereva wa lori la trela ambaye bado hajatambuliwa, alikuwa analiendesha akielekea upande wa mji wa Mai Mahiu ajali hiyo ilipotokea,” ripoti hiyo ya polisi ilisema.

Kufika eneo la VIP karibu na Mai Mahiu, dereva huyo wa lori la trela alishindwa kulidhibiti na likagonga matatu aina ya Toyota Hiace  la sacco ya Murang’a-Nairobi almaarufu Muna.

Ripoti hiyo ilisema kwamba trela hilo liligonga magari mengine mawili hivyo basi kuifanya ajali kuwa iliyohusisha magari manne.

“Waliopoteza maisha yao ni wanawake watano, wanaume watatu na mtoto mmoja wa kike. Nao wanawake watano na wanaume watatu walipata majeraha mabaya na wakakimbizwa hospitalini ambako wamelazwa,” ripoti hiyo ikaeleza.

Iliongeza kwamba uchunguzi kamili wa hali na mazingira ya ajali hiyo umeanzishwa.

Tayari magari yote yaliyohusika katika ajali hiyo yamepelekwa katika kituo cha polisi ili ukaguzi ufanywe.