Watu wa Rais waingia baridi

Watu wa Rais waingia baridi

JUSTUS WANGA na BENSON MATHEKA

BAADA ya kushindwa kwenye uchaguzi mdogo wa kiti cha eneobunge la Kiambaa, washirika wa Rais Uhuru Kenyatta katika chama cha Jubilee wameingiwa baridi na sasa wanapanga kukutana Jumatano kupanga upya mikakati ya kukabiliana na umaarufu wa Naibu Rais William Ruto eneo la Mlima Kenya.

Hatua hii ya haraka inachangiwa na hofu ya kupoteza viti vyao huku umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya ukiongezeka hasa uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

Mkutano huo utakaofanyika katika makao makuu ya chama cha Jubilee eneo la Pangani, Nairobi utajadili mbinu za kumzima Dkt Ruto ambaye umaarufu wake eneo la Kati umefanya umaarufu wa Rais Kenyatta katika ngome yake kuonekana kushuka pakubwa.

Baadhi ya watetezi shupavu wa Rais Kenyatta akiwemo Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru wamelalamika vikali wakitaka mabadiliko katika usimamizi wa chama cha Jubilee kufuatia kuendelea kuaibishwa kwa kubwagwa katika chaguzi ndogo kadhaa.

“Wafuasi halisi wa Jubilee hawana furaha na hatua za dharura zinafaa kuchukuliwa kuzuia kisiporomoke,” alisema Waiguru.

Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba baadhi ya washirika wanataka Rais Kenyatta kuwahakikishia kwamba wanaweza kumtegemea sasa, kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 ili wasipoteze kura zao.

Akiwa rais anayestaafu na ngome yake ikiwa imegawanyika, wadadisi wanasema Rais Kenyatta amejipata pagumu.

Imeibainika kuwa hata kabla ya uchaguzi mdogo wa Kiambaa na Wadi ya Mugug Alhamisi wiki hii, Idara ya Taifa ya Ujasusi (NIS) ilikuwa imeonya Rais Kenyatta kuwa Jubilee ingeshindwa kwa sababu zilizozidi uwezo wa ofisi ya Jubilee.

Hasira za wapigakura kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na kumtenga Dkt Ruto, na hatua ya Rais Kenyatta kumkumbatia kiongozi wa ODM Raila Odinga imechangia kushuka kwa umaarufu wa chama cha Jubilee.

Baadhi ya washirika wa sasa na wa zamani wa Rais wanahisi kwamba wakati umefika wa kubadilisha usimamizi wa chama ili kuleta “damu mpya”.

Kulingana na Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata ambaye ni mmoja wa viongozi walioasi Jubilee eneo la Mlima Kenya, Rais Kenyatta anapotoshwa na washauri na washirika wake wa kisiasa.

“Tishio la Mlima Kenya kugawanyika lipo lakini tunaweza kuepuka kupitia Rais kukubali ukweli, kuja kwetu na kupokea maoni yetu kuhusu siasa za urithi na malalamishi ya uchumi ambayo yalifanya watu wetu kumuasi,” alisema Kang’ata.

Alisema muhimu kabisa katika kupatanisha eneo hilo ni Rais Kenyatta kukubali kuwa Dkt Ruto amepenya eneo la Mlima Kenya na kwamba wakazi hawafurahishwi na sera zake za uchumi na kukatiza ushirikiano wake na Bw Odinga.

“Wanafaa (washirika wa Rais) kuacha muungano wanaosuka na ODM na kukoma kujaribu kumuunga Bw Odinga kugombea urais,” alisema.

Taifa Jumapili ilibaini kwamba baadhi ya washauri wa Rais wanataka asimamishe mipango ya Jubilee kuungana na ODM kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wiki jana, Bw Tuju alisema kwamba ni Rais aliyeagiza mazungumzo ya kuunganisha chama tawala na ODM.

Baadhi ya washirika wa Rais wanapendekeza arejeshe uhusiano wake na Dkt Ruto, jambo ambalo wadadisi wa siasa wanasema linaweza kuwa mlima kwake.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa Dkt Godwin Siundu, njia bora ya Rais Kenyatta ni kujiondoa katika siasa za urithi alivyofanya mtangulizi wake Mwai Kibaki na kuwaacha wakazi kujiamulia.

Anasema hofu ya Rais kuidhinisha mmoja wa vinara wa NASA imefanya washirika wa Dkt Ruto kuvuruga mambo katika ngome yake ya Mlima Kenya.

You can share this post!

Mwingine akiri kunajisi na kunyonga wasichana 5 Moi’s...

Mombasa yasitisha mashindano ya ndondi hadi michezo ya...