Kimataifa

Watu wachache kualikwa kuhudhuria hafla ya Biden kuapishwa

December 17th, 2020 2 min read

Na XINHUA

WASHINGTON D.C., Amerika

KAMATI ya Bunge la Congress ambalo linahusika na mchakato wa maandalizi ya sherehe za kumwaapisha Rais Mteule Joe Biden, Alhamisi ilisema ni wageni wachache tu watakaoruhusiwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na kupanda kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Rais mteule Biden ataapishwa Januari 20, 2021 jijini Washington japo ni wageni wachache tu kutoka ndani na nje ya nchi watakaoruhusiwa kuhudhuria hafla hiyo.

Amerika ni kati ya nchi ambazo ziliathiriwa vibaya na virusi vya corona, na wadadisi wa kisiasa wanasema kushindwa kwa utawala wa Rais Donald Trump kukabili ugonjwa huo ndiko kulikochangia pakubwa kushindwa kwake katika uchaguzi ulioandaliwa mwezi uliopita.

Kulingana na Kamati Jumuishi ya Bunge la Congress (JCCIC) ambayo huhusika na sherehe za upokezanaji wa mamlaka, kila seneta atapokezwa mwaliko pamoja na mgeni mmoja kutoka jimbo lake.

Kwa jumla ni mialiko 1,070 ambayo itatolewa kwa maseneta.

“JCCIC baada ya kushauriana na wataalamu wa kimatibabu na afya ya umma pamoja na kamati inayosimamia hafla ya uapisho wa Rais, imeamua kwamba idadi ya wageni watakaohudhuria kuapishwa kwa Rais Mteule Joe Biden, ijumuishe watu wachache.”

“Hii ni kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona si tu Marekani bali hata katika mataifa mengine duniani,” akasema mwenyekiti wa JCCIC, Seneta Roy Blunt kupitia taarifa. Hii itakuwa hafla ya 59 ya kumwaapisha Rais ambayo kwa kawaida huhudhuriwa na halaiki ya raia pamoja na Marais waalikwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Miaka ya nyuma, kamati hiyo ya Congress ingetoa tiketi 200,000 kwa wageni na kuwapa maseneta nyingine za kuwapa wakazi wachache wa majimbo yao ili wahudhurie sherehe hizo.

Mnamo Jumanne, kamati ya Ikulu inayopanga hafla hiyo kwa ushirikiano na JCCIC, iliwataka raia wa Marekani wafuatilie hafla hiyo nyumbani kupitia runinga zao badala ya kufika jijini Washington moja kwa moja.

Kupunguzwa kwa idadi ya wanaohudhuria sherehe za uapisho kunaonyesha kujitolea kwa Biden na Makamu wa Rais mteule Kamala Harris kusaidia taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi duniani kushinda vita dhidi ya virusi vya corona.

Mnamo Jumanne, kikosi cha Biden kilitangaza kuwa Rais huyo ataapishwa Mashariki mwa mji wa Washington DC.

Biden mwenyewe amewarai raia wa Marekani wasalie nyumbani na kufuatilia uapisho wake kwenye runinga.