Watu wachache wajitokeza kujiandikisha IEBC ikisaka kura 4.5m

Watu wachache wajitokeza kujiandikisha IEBC ikisaka kura 4.5m

Na KENYA NEWS AGENCY

DALILI za mapema zinaonyesha kwamba huenda Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ikakosa kusajili wapiga kura wapya 4.5 milioni katika awamu ya pili ya shughuli hiyo, iliyoanza Jumatatu.

Hii ni kwa sababu siku tatu baada ya shughuli hiyo kuanza, ni watu wachache zaidi wamesajiliwa kote nchini ikilinganishwa na idadi lengwa.

Katika Kaunti ya Kakamega, meneja wa uchaguzi katika kaunti hiyo, Bi Grace Rono, alisema IEBC inalenga kusajili wapigakura wapya 225,199 .

Lakini kufikia jana, makarani wa tume hiyo waliwasajili watu 57,816 pekee.

Akiongea na wanahabari nje ya afisi yake mjini Kakamega, afisa huyo aliongeza kuwa ni wapigakura 17,819 wamebadili vituo vya kupigia kura.

“Idadi ya watu wanaojitokeza kujisajili ingali ndogo zaidi hali inayoibua hofu kwamba huenda tusiweze kufikisha idadi lengwa ya wapigakura 225,199 wapya. Tunawaomba wanasiasa na viongozi wa kidini na wadau wengine kuendesha uhamasisho ili watu wengi wajitokeze,” akasema Bi Rono ambaye aliandamana na Mbunge Mwakilishi Kike wa Kakamega, Bi Elsie Muhanda.

Katika Kaunti ya Laikipia ni wapigakura wapya 274 ambao walikuwa wamesajiliwa tangu Jumatatu huku kaunti hiyo ikilenga kusajili watu 63, 725 ndani ya siku 20 zijazo.

Akiongea na wanahabari Jumanne mjini Nanyuki, mshirikishi wa IEBC Kaunti ya Laikipia, Bi Agnes Mutisya, aliwahimiza wakazi kujitokeza wasajiliwe ndiposa waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

“Natoa wito kwa vijana wajitokeze kwa wingi ili tuweze kutimiza idadi ya wapigakura wapya tuliowalenga,” akasema.

Bi Mutisya alieleza kuwa katika awamu ya kwanza ya shughuli hiyo mwaka jana, walisajili jumla ya wapigakura wapya 11,605 ilhali walilenga wapiga kura 75,330.

Katika Kaunti ya Kisumu, viongozi walitoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi ili wajisajili kuwa wapigakura.

Wakati wa uzinduzi wa shughuli hiyo katika ukumbi wa kijamii wa Mama Grace Onyango, Spika wa bunge la Kaunti, Bw Elisha Oraro alisema uhamasisho unafaa kuendeshwa hadi ngazi ya vijijini.

Meneja wa uchaguzi Kaunti ya Kisumu, Bw Patrick Odame, alisema kando na wanasiasa, uhamasisho unafaa kuendeshwa na viongozi wa kidini na wale wa mashirika ya kijamii.

“Tunataka kufikia siku ya mwisho ya awamu hii ya usajili wa wapigakura wapya, tunatarajia kuwa tumewasajili jumla ya wapigakura 250,000 zaidi,” akasema Bw Odame.

Kaunti zingine ambako idadi ndogo ya watu wamejitokeza kujisajili kuwa wapiga kura wapya ni Kisii, Homa Bay, Mombasa, Siaya, Narok, Machakos.

Seneta wa Kisii, Profesa Sam Ongeri alilalamikia idadi ndogo ya watu waliojitokeza kwa shughuli hiyo katika eneo bunge la Bonchari.

Akiwahutubia wajumbe wa ODM katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo (ATC) mjini Kisii, Ongeri aliwahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Mradi wa maji Nakuru haujakamilika kama...

Dhuluma zinadumaza wanawake kisiasa – Ripoti

T L