Habari za Kitaifa

Watu wafia majumbani madaktari wakigoma

April 17th, 2024 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAGONJWA wanaendelea kupoteza maisha kwa wingi nyumbani kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea kote nchini.

Familia ya Maxwel Maronda inahuzunika ikikumbuka jinsi mpendwa wao aliyekuwa na umri wa miaka 24 alivyofariki baada ya madaktari wanaogoma kukataa kumhudumia.

Maronda alianza kuugua siku ambayo madaktari walianza mgomo na akahudumiwa katika hospitali kadhaa za kibinafsi na kugunduliwa alikuwa na tatizo la damu.

Alizidiwa na kupelekwa katika hospitali ya Mama Lucy iliyo karibu na nyumba yao mtaani Saika ambapo alihudumiwa lakini akazidiwa siku chache baadaye.

Maxwel alifariki akiwa katika hospitali ya Kijabe alikopelekwa baada ya hali yake kuwa mbaya na familia yake ilisema hangepona iwapo madaktari hawangekuwa kwenye mgomo.

“Tulikuwa tukiomba madaktari watusaidie. Walikuwa wamegoma na hakukuwa na yeyote wa kutushauri,” alisema dada ya marehemu Jilian Bosineri.

“Tunahitaji madaktari hawa. Sio Maxwell alikufa peke yake. Mtu mwingine aliyelazwa karibu akiwa Mama Lucy alifariki. Serikali haifai kuruhusu madaktari kuandamana. Inafaa kuwashughulikia.

Hospitali ya Jaramogi Oginga

Katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga (JOOTRH), mhudumu wa afya ambaye hakutaka jina lake litajwe aliripoti kwamba vifo vya wagonjwa vimeongezeka kutokana na ukosefu wa madaktari.

Alisema kwamba hospitali hiyo imepata shida kubwa kutokana na ukosefu wa wahudumu wa afya na kuongeza huwa imesitisha huduma kwa wagonjwa wanaougua magonjwa sugu ikiwemo saratani.

Hii ni licha ya Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt Richard Lesiyampe kusema kuwa wamelazimika kutegemea wakuu wa idara, wauguzi na wataalamu 84 kutoa huduma muhimu na za dharura.

“Tunaendelea kufanya kazi lakini katika mazingira magumu sana,” alisema, huku akitoa wito wa kusitishwa kwa haraka kwa mzozo unaotishia kusambaratisha utoaji wa huduma za afya.

Mwezi uliopita, hospitali hiyo iliwaomba wananchi kuchukua miili ambayo imekwama katika mochari ya hospitali hiyo.

Dkt Lesiyampe alialika watu waliomepoteza jamaa zao kutembelea hospitali hiyo kuanzia Machi 17 ili kutambua miili hiyo kabla ya kuzikwa katika makaburi ya kaunti hiyo katika muda wa siku 21.

Huku wagonjwa wakiendelea kufariki, serikali imekataa matakwa ya madaktari ikisema haina pesa na lazima wajifunze kuishi kulingana na uwezo wao.

Kote nchini, hata hivyo, madaktari wanasisitiza kwamba wanapaswa kulipwa kile wanachostahili chini ya makubaliano ya pamoja ya 2017 ambayo yaliongeza mishahara na marupurupu yao.

Wanasema serikali inaweza kumudu kuwalipa lakini haipatiii huduma ya afya kipaumbele.

Jana, Baraza la Magavana lilisema hata kama Serikali ya Kitaifa itakubali matakwa ya madaktari, hawa pesa za kuwalipa.

Katika nyumba zao, mbali na macho ya umma,maelfu ya wagonjwa wanakufa. Wengine wataishi, wengine kama Maxwell hawatapona.

RIPOTI ZA HELLEN SHIKANDA NA ANGELINE ACHIENG