Habari

Watu wanane wakiwemo maafisa kadha wakamatwa Matungu kwa kukiuka sheria na kanuni za KCPE

October 30th, 2019 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

MAAFISA kadha ni miongoni mwa watu wanane katika kaunti ndogo ya Matungu, Kaunti ya Kakamega waliokuwa wamepewa wajibu kusimamia shughuli ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE 2019), wanazuiliwa kuhojiwa na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kakamega kuhusu udanganyifu na ukiukaji mwingine wa sheria na kanuni za mtihani.

Wanane hao ni pamoja na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Ngairwe ambaye pia ndiye meneja wa kituo Washington Magero, nyapara msimamizi na waangalizi sita wa watahiniwa.

Wanazuiliwa baada ya kupatikana na simu katika vyumba vya mitihani pamoja na kuwaruhusu walimu watatu kuingia shuleni wakati mnamo ambapo wako likizoni mnamo Jumanne, Oktoba 29, 2019.

Baraza la Mitihani ya Kitaifa Nchini (Knec) liliorodhesha simu na vifaa vingine kadhaa vya kielektroniki kuwa ni marufuku kwa watahiniwa, nyapara wasimamizi, na waangalizi wa watahiniwa katika vyumba ambavyo vinatumika mahususi kwa ajili ya mitihani.

Wajifanya wapishi

Walimu watatu: Edwin Keya, Ferdinand Balungu, na Scolastica Osodo walikamatwa kwa kujifanya wapishi shuleni humo.

Maafisa wa polisi walichukua hatua hiyo baada ya afisa wa Knec aliyekuwaakifuatilia shughuli shuleni humo kubainisha kulikuwa na matukio ya kutiliwa shaka.

Aliripoti kisa hicho kwa manyapara wasimamizi wenye ngazi za juu na OCS Bw Samuel Kinoti na Kamanda wa CIPU Shem Nyamongo walifika katika shule hiyo ambapo waliwakuta walimu hao watatu wakijifanya ni wapishi shuleni.

Kwa mujibu wa afisa wa usalama wa ngazi ya juu katika kaunti, walimu hao watatu na mwalimu mkuu – Magero – walipelekwa katika kituo cha polisi cha Matungu kuandikisha taarifa na kuhojiwa.

Kamishna wa Kaunti ya Kakamega Pauline Ndola amesema mkuu wa kituo, manyapara na waangalizi wa watahiniwa na wengine wasioruhusiwa kituoni lakini waliopatikana hapo wanachunguzwa.

“Maafisa wa uchunguzi wanafuatilia kisa hiki na tayari tumepata wengine mbadala. Nimezuru shule hiyo na nawahakikishieni kwamba kila kitu kimeendelea ipasavyo,” amesema Bi Ndola.