Kimataifa

Watu wanne wafariki baada ya kukanyaga kilipuzi

February 12th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

BAMAKO, MALI

JESHI la Mali limesema kwamba watu wanne waliuawa na kadhaa wakajeruhiwa baada ya gari lao kulipuliwa eneo la kati la mkoa wa Mopti.

Jeshi lilisema watu hao walikuwa wakitoka sokoni Ijumaa gari lao lilipokanyaga kilipuzi kati ya Kontza na Dera mkoa wa Mopti.

Shambulio hilo lilijiri wiki chache baada ya watu 26 wakiwemo watoto na wanawake, kuuawa baada ya gari lao kulipuliwa karibu na mpaka wa Burkina Faso wakielekea sokoni.

Hakuna kundi lililokiri kuhusika na mashambulio hayo ingawa magaidi wanaoshirikiana na mtandao wa Al-Qaeda huwa wanatega vilipuzi kulenga wanajeshi wa Mali.

Mnamo Januari 27, magaidi wa Kiislamu walivamia kambi ya kijeshi Kaskazini mwa Mali na kuuawa wanajeshi wanne.