Habari Mseto

Watu watatu wahofiwa kukwama kwa vifusi vya maporomoko Kimende

May 15th, 2024 2 min read

CHARLES WASONGA Na SIMON CIURI

WATU watatu wanahofiwa kukwama ndani ya vifusi vya maporomoko ya ardhi yaliyotokea Kimende, eneobunge la Lari, Kaunti ya Kiambu.

Maporomoko hayo yalitokea Jumanne usiku na waathiriwa wanasemekana kuwa walikuwa wakielekea nyumbani baada ya shughuli za siku walipofunikwa na vifusi.

Jumatano asubuhi Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi amezuru eneo hilo huku juhudi za uokoaji zikishika kasi.

Msako wa kuwatafuta walionaswa kwa maporomoko unaongozwa na maafisa wa kukabiliana na majanga na masuala ya dharura wa serikali ya Kaunti ya Kiambu wakishirikiana na wafanyikazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini (Kenya Red Cross – KRC).

“Pamoja na maafisa wa kukabiliana na majanga wa kaunti, tulitembelea eneo hilo ili kutathmini hali ilivyo na kuwasaidia wakazi walioathirika, huku operesheni ya kuwatafuta watu ambao haijulikani waliko ikiendelea. Tunashauriana na halmashauri za barabara zilizo chini ya serikali kuu ili kuona ikiwa muundo wa barabara unaweza kuboreshwa ili kuepuka janga kama hili siku zijazo,” gavana Wamatangi akasema.

Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi awasili katika eneo la maporomoko ya ardhi Kimende. PICHA | SIMON CIURI

Mkuu huyo wa kaunti wakati uo huo aliwataka wenyeji wanaoishi katika maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi kuondoka kwa kuahidi kuwapa msaada wa kibinadamu.

“Tunawataka wakazi wanaoishi katika maeneo hatari yanayokabiliwa na maporomoko ya ardhi kuhamia maeneo salama. Serikali ya Kaunti inatoa usaidizi wa kibinadamu kwa wale wote walioathiriwa na janga hilo la kiasili,” akaongeza.

Mnamo Jumanne KRC, kwenye taarifa fupi, ilisema ilikuwa imetuma wahudumu wake katika eneo la mkasa.

“Maporomoko ya ardhi yametokea katika bonde la Kimende katika kaunti ya Kiambu. Inahofiwa kjuwa watu kadhaa wamekwama huko,” KRC ikasema.

“Kikosi chetu kiko njiani kuelekea eneo la mkasa,” taarifa hiyo iliongeza.

Inaaminika kuwa mkasa huo ulitokea kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa katika eneo hilo na maeneo ya karibu.

Mkasa huo unafuata tukio jingine ambapo watu karibu 60 waliaga dunia katika eneo la Mai Mahiu baada ya nyumba zao kuangukiwa na maporomoko ya ardhi na kusombwa ma maji ya mafuriko.

Serikali imetoa wito kwa watu kuondoka katika maeneo yanayokaribiana na mito na maeneo yenye hatari ya kutokea kwa maporomoko ya ardhi.

Kufikia sasa jumla ya watu 289 wameaga dunia kote nchini kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Haya ni kwa mujibu wa takwimu alizotoa Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura mnamo Jumanne.