Habari za Kitaifa

Watu wawili waaga dunia kufuatia ajali ya ndege mbili jijini Nairobi

March 5th, 2024 1 min read

NA DANIEL OGETTA

POLISI wanachunguza ajali ya ndege mbili zilizogongana juu hewani Jumanne asubuhi jijini Nairobi.

Ndege ya Safarilink iliyokuwa ikielekea Diani katika Kaunti ya Kwale, imelazimika kutua uwanjani Wilson kwa ukaguzi kufuatia ajali hiyo na ndege nyingine ya 99 Flying Club.

Watu wawili waliokuwa wameabiri ndege ya  99 Flying Club wamepoteza maisha wakati wa ajali hiyo, polisi wameambia Taifa Leo.

Safarilink imethibitisha kutokea ajali hiyo ya mwendo wa saa nne kasorobo.

“Ndege yetu nambari 053 iliyokuwa na abiria 39 na wafanyakazi watano imepata ajali ikipaa. Hali hiyo imelazimu ndege kurejea uwanjani Wilson na wote waliokuwa ndani wako salama,” umesema usimamizi wa Safarilink.

Tayari usimamizi umevifahamisha vyombo husika vya usalama vinavyoendelea na uchunguzi.

99 Flying Club ni shule ya uchukuzi wa ndege inayoshughulikia mashirika ya kibinafsi, mashirika ya ndege na uchukuzi wa kibiashara.