Habari

Watu zaidi ya nusu milioni Nakuru hawakujitokeza kupata Huduma Namba

May 29th, 2019 2 min read

NA PHYLLIS MUSASIA

ZAIDI ya watu nusu milioni wanaoishi katika Kaunti ya Nakuru, walikosa kushiriki shughuli ya kukiandikisha ili kupokea Huduma Namba.

Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuongeza muda wa wiki moja zaidi kuhakikisha hakuna mkazi wa taifa hili – mwenyeji au mgeni – anaachwa nyuma.

Takriban watu 629, 542 katika Kaunti ya Nakuru hawakujiandisha kamwe.

Kulingana na kamishina wa Nakuru Bw Erustus Mbui, wale waliojitokeza katika shughuli hiyo iliyokamilika Jumamosi, Mei 25, 2019, ni watu 1.7 milioni kati ya jumla ya watu wa 2.3 milioni wa Nakuru.

“Baada ya kukamilika kwa shughuli, tulibainisha tumerekodi jumla ya watu 1,702,086 milioni. Kwetu sisi ni idadi nzuri ambayo inawakilisha asilimia 73. Wale ambao hawakufika katika vituo watalazimika kusafiri hadi maeneo yao walikozaliwa ili kufanya hivyo kupitia afisi za machifu,” akaeleza Bw Mbui.

Hata hivyo, muda wa wiki moja ulioongezwa na Rais Kenyatta uliwezesha watu takriban 300,000 kujiandisha kwenye kaunti hiyo kwani rekodi za hapo awali zilionyesha kuwa idadi ya watu waliokuwa wamejisajili ilikuwa 1.4 milioni.

“Tunashukuru sana kwa muda ambao Rais aliagiza uongezwe wakati wa shughuli hiyo. Idadi ya watu ambao walikuwa wamejisajili Nakuru ilikuwa imekwamia watu 1.4 milioni; kuashiria asilimia 62.25,” akasema.

Bw Mbui amesema afisi yake ilifanya kila juhudi kueneza ujumbe kuhusu umuhimu wa nambari hiyo.

Baadhi ya wanasiasa na viongozi wa makanisa walilaumiwa kueneza propaganda kuhusu Huduma Namba.

Kamishina hata hivyo amesema viongozi hao hawakufaulu katika njama yao kwani idadi ya wale waliojiandikisha ilikuwa ya juu kinyume na jinsi walivyotarajia.

“Kulikuwa na habari nyingi sana ambazo hazikuwa za kweli zilizoenea kukandamiza shughuli nzima. Wanasiasa wengi walieneza porojo kwa wakazi kuhusu Huduma Namba lakini ofisi yangu ilikuwa ngangari kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inaendelea kama ilivyokuwa imeratibiwa,” akaeleza Bw Mbui.

Mwanzoni mwa shughuli hiyo changamoto nyingi kama vile mashine kutatizika kwenye baadhi ya maeneo zilitatiza sana shughuli.

Wakazi wengine pia walionekana kukosa stakabadhi muhimu zilizohitajika kutumika kwenye shughuli hiyo kama vile vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho.

“Tulitumia watu kama vile maajenti, wafanyabiashara kule sokoni, baadhi ya makanisa na pia wanabodaboda kutusaidia kueneza jumbe bora na sahihi kuhusiana na umuhimu wa watu kujisali. Haikuwa rahisi lakini tulipambana sana,” akasema.

Baadhi ya wakazi waliokuwa kwenye foleni Jumamosi ili kujiandikisha wasije wakafungiwa nje wakati wa mwisho walisema walifanya hivyo baada ya kupata habari kuhusu umuhimu wake.

Wengine walisema walikuwa wamebanwa na kazi na kupata muda wa kujisali ikawa changamoto.

“Nina ufahamu kuwa leo ni siku ya mwisho ya kujisali. Ninashukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata fursa ya kuwa miongoni mwa wale ambao wamejisali. Kazi ninayofanya mara nyingi huwa hainipi nafasi lakini leo nimefaulu,” akaelezea Bw Evans Kimutai baada ya kujiandisha Jumamosi jioni.

Bi Khadija Salama ambaye pia alikuwa miongoni mwa wale ambao waling’ang’ana kwenye foleni siku hiyo wasije wakafungiwa nje, alilaumu viongozi wa siasa kwa kumpotezea muda mwingi kabla ya kuamua kujisajili.

“Viongozi wetu wanapaswa kueneza mambo yanayotusaidia na sio kutupumbaza,” akasema Bi Salama.