Habari Mseto

Watuhumiwa wa NYS waonywa dhidi ya kuvuruga ushahidi

November 22nd, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mkuu Bw Douglas Ogoti Alhamisi aliwaamuru mawakili wanaowatetea washukiwa 37 katika kashfa ya Sh226 milioni ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) wamwache mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) aendeleze kesi hiyo bila kusumbuliwa.

Bw Ogoti alitoa agizo hilo baada ya mawakili kuendelea kuteta kwamba hawajakabidhiwa nakala za ushahidi katika kesi hiyo inayowakabili aliyekuwa katibu mkuu wizara ya ugatuzi Bi Lillian Omollo.

Wengine alioshtakiwa nao ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa NYS Richard Ethan Ndubai , wafanyabiashara Anne Wambere Wanjiku Ngirita , Phyilis Njeri Ngirita, Lucy  Wambui Ngirita na Jeremiah Gichiri Ngirita na pia wafanyakazi wa ngazi za juu NYS.

“Naamuru mawakili wanaowasilisha maombi ya kila namna wamwache DPP aendeleze kesi hii jinsi anavyoelewa,” Bw Ogoti aliwaamuru mawakili.

Na wakati huo huo Bw Ogoti aliwataka mawakili wawatetee washtakiwa jinsi wanavyoelewa.

“Kila upande ufanye kesi bila kuvurugana,” alisema Bw Ogoti akiongeza , “Ikiwa kutatokea kasoro katika uendelezaji wa kesi hii basi sheria iko na suluhu ya masuala yote.”

Bw Ogoti alitoa uamuzi huo baada ya mawakili kumweleza hakimu kuwa hawakuwa wamepewa nakala za ushahidi wa malipo yaliyotolewa kwa Bi Phyilis  Njeri Ngirita na kampuni yake Njewanga Enterprises.

Ubishi mkali ulizuka baada ya mawakili kumweleza hakimu kuwa hawakuwa wamekabidhiwa nakala za  ushahidi aliokuwa akitoa afisa mkuu wa ununuzi na usambazaji wa bidhaa wizara ya ugatuzi Bw  Sebastian Mokua.

Mawakili hao waliomba kesi isimamishwe wapewe nakala za ushahidi huo.

Washukiwa 37 wa kashfa ya NYS ya Sh226m wakiwa kortini Novemba 22, 2018. Picha/ Richard Munguti

Baada ya majimbizano makali kati ya mawakili wanaowatetea washtakiwa na  viongozi wa mashtaka Jalson Mokaya ,Caroline Kimiri na Evah Kanyuira  hakimu aliamuru kila pande iendeleze kesi bilaz kuingiliwa.

Viongozi hao wa mashtaka  waliwakabidhi kila mshukiwa nakala ya ushahidi wakiongozwa na aliyekuwa katibu mkuu Bi Lillian Mbogo Omollo.

Mabunda ya nakala hizo yakiwa yameandikwa majina ya washukiwa yalitandazwa katika ukumbi ambapo kesi hiyo inaendelea.

“Nimewasilisha ushahidi uliotakiwa,” Bi Kimiri alimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti.

Bi Kimiri aliomba mahakama iwaamuru washukiwa wote wachukue nakala za mashahidi wawakabidhi mawakili wanaowatetea.

Lakini baada ya muda kidogo wakati afisa mkuu wa masuala ya ununuzi wa bidhaa wizara ya ugatuzi Bw Sebastian Mokua alipoanza kutoa ushahidi iliimbuka kuwa nakala ya ushahidi aliyokuwa anasoma haikuwa imekabidhiwa washtakiwa ndipo kizugumkuti kipya kikazuka.

Mawakili Danstan Omari, Assa Nyakundi na Peter Kabue wakasimama na kueleza mahakama kuwa.

Washukiwa hao 37 wamekanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana. Kesi inaendelea.