Habari Mseto

Watumiaji barabara ya Lamu-Mombasa walalamikia ongezeko la vizuizi vya maafisa

January 29th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MADEREVA na abiria wa mabasi ya usafiri wa umma yanayotumia barabara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa wanaiomba idara ya usalama eneo hilo kupunguza idadi ya vizuizi vya polisi eneo hilo wakidai vinachangia safari zao kucheleweshwa.

Bararbara kuu ya Lamu kuelekea Mombasa ina takriban vizuizi vitano vya barabarani, cha kwanza kikiwa ni kile cha Ndeu ilhali vizuizi vingine vikipatikana maeneo ya Witu, Gamba, Itsowe na Minjila.

Ni katika vizuizi hivyo ambapo abiria hutakiwa kushuka pamoja na mizigo yao ili kukaguliwa kwanza kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari zao.

Katika mahojiano na wanahabari Jumanne, watumiaji wa barabara hiyo walilalamika kuwa katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakifika sehemu zao kuchelewa kutokana na muda mwingi unaopotezwa barabarani hasa kwenye vizuizi hivyo.

Bw Mohamed Athman alisema anaamini ikiwa vizuizi hivyo vitapungua, wasafiri wataweza kufika sehemu zao mapema kinyuma na sasa.

Kwa kawaida, safari za kutoka Lamu hadi Mombasa huchukua kati ya masaa sita na saba kufika, lakini tangu vizuizi hivyo kuwekwa barabarani, muda wa kusafiri umeongezeka hadi masaa manane au tisa.

Bw Athman alisema maafisa wa polisi na jeshi wanaokagua abiria kwenye vizuizi huchukua kati ya dakika 20 hadi 30 kwa kila kizuizi, jambo ambalo pia alidai linawachokesha wasafiri.

“Vizuizi vimekuwa vingi mno. Muda mwingi unapotezwa vizuizini. Ni vyema vizuizi vipunguzwe ili pia kupunguza muda utumikao kukagua abiria na mizigo yao barabarani. Wasafiri wanahitaji kufika sehemu zao kwa wakati ufaao badala ya kuchelewa kila siku,” akasema Bw Athman.

Bi Amina Abdallah alipendekeza kwamba maafisa wa usalama wawakague abiria ndani ya magari wanayosafiria badala ya kuwataka kubebana na mizigo na kushuka ili wakaguliwe.

Bi Abdallah alisema hatua hiyo imesababisha dhiki hasa kwa akina mama wajawazito, wazee na wagonjwa ambao kila mara huzidiwa wanaposafiri barabarani.

“Tungeomba idara ya usalama kufanyia mageuzi shughuli ya upekuzi wa abiria barabarani. Badala ya kutuamuru kushuka kila eneo la kizuizi tukiwa na mizigo yetu ili tukaguliwe, shughuli hiyo ifanyiwe ndani ya magari. Kutushukishashukisha kila mara ilhali tuko na wazee, akina mama wajawazito na wagonjwa huko ni kutusababishia dhiki,” akasema Bi Abdallah.

Baadhi ya watumiaji wa barabara hiyo aidha walikinzana kimaoni, ambapo wengine waliipongeza hatua ya kuwekwa vizuzizi vya polisi barabarani wakisema inasaidia kudhibiti vilivyo usalama wa eneo hilo.

“Sioni makosa kuwekwa vizuizi vya barabarani. Heri tuchelewe safarini lakini tufike salama. Usalama wa barabara yetu hauaminiki bado. Ikiwezekana vizuizi viongezwe hasa,” akasema mmoja wa uringo wa mabasi ya usafiri wa umma yanayotumia barabara ya Lamu-Mombasa, Bw Athman Salim.

Bi Loice Kirathe alisema mbali na vizuizi vya barabarani, idara yausalama pia iongeze doria kwenye barabara hiyo.

Kwa upande wake aidha, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia aliwataka wote wanaotumia barabara ya Lamu-Mombasa ambao analalamikia mpangilio wa usalama kukubali mabadliko hayo.

“Wafahamu kwamba hatua yoyote inayochukulia ya kiusalama huwa ni ka manufaa yao.Serikali lazima ilinde watu wake. Badala ya kulalamika, wakubali tu,” akasema Bw Macharia.