Watumiaji mitandao ya kijamii wafurahia mvua siku ya kwanza 2021

Watumiaji mitandao ya kijamii wafurahia mvua siku ya kwanza 2021

Na SAMMY WAWERU

MVUA ilishuhudiwa katika maeneo tofauti ya nchi kuanzia usiku wa kuamkia Alhamisi, Desemba 31 iliyokuwa siku ya mwisho ya mwaka wa 2020.

Baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii, wameeleza kuridhishwa na mfungo wa aina hiyo wa mwaka, wakiutaja kama baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutanguliza 2021.

Manyunyu ya mvua yalianza kushuhudiwa usiku wa manane, mnamo Alhamisi. Ni hali iliyoendelea kushuhudiwa Ijumaa, Januari 1, mwaka 2021 uking’oa nanga.

Maeneo yafuatayo yametajwa kupokea mvua kwa kiwango kilichopitiliza, na mengine ya kadri; Kisumu, Nyeri, Machakos, Uasin Gishu, Murang’a, Kajiado, Taita Taveta, Kericho na Nyandarua.

Orodha ya sehemu zilizoshuhudia mvua pia inajumuisha Kiambu, Makueni, Nairobi, Nakuru, Embu, Tharaka Nithi, Meru, Kitui, Turkana, Samburu, Kirinyaga, kati ya maeneo mengine.

Watumiaji mitandao ya kijamii walikuwa na maoni yao kuelezea hali hii.

“Mungu ni Mkuu, twashukuru,” akachapisha @Gregory Mutwiri kwenye Facebook.

“Nyandarua tumebarikiwa,” akasema @Kevvyn Bianga.

Kulingana na Joab Mako Odhiambo, maeneo mengi Kaunti ya Kisumu yameshuhudia mvua ya mawe. “Kisumu ni mvua ya mawe,” Odhiambo akaelezea, akichapisha picha inayoonyesha hali ilivyokuwa.

“Kibwezi, Makueni mvua inaendelea kunyesha,” Nason Munyao akasema.

“Mvua iliyonyesha Machakos imenishtua,” akaongeza @Susan Mutuku.

Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajakuwa na mvua kama vile Pokot Magharibi, Trans Nzoia, Narok, Kakamega, kati ya mengineyo.

“Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia ni kavu,” Ruth Waweru akadokeza.

Kutokana na mvua iliyoshuhudiwa, baadhi wamezua ucheshi wakihoji imesafisha na kuondoa mazito na magumu yaliyoshuhudiwa 2020, janga la Covid-19.

“Mwaka wa 2020 unakoga ili kukaribisha baraka za 2021,” @Tony Chebe Kang’ara akaelezea.

You can share this post!

WEST HAM YAPIGA EVERTON: Kocha Moyes aangusha waajiri wake...

Mataifa 16 yathibitisha kushiriki tenisi za kimataifa...