Watumishi wa serikali wasusia mikopo ya magari

Watumishi wa serikali wasusia mikopo ya magari

Na KENYA NEWS AGENCY

MAAFISA wa serikali ya kitaifa wamesusia hazina iliyoanzishwa na serikali kuwapa mikopo ya kununua magari, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Mishahara (SRC) Ann Gitau amefichua.

Kufikia wakati huu, ni maafisa 100 pekee waliochukua mikopo ya jumla ya Sh180 milioni tangu hazina hiyo ilipoanzishwa mnamo 2014. Hazina hiyo ilitengewa Sh3.8 bilioni ilipoanzishwa.

Akizungumza Jumanne akiwa Kapsabet, Kaunti ya Nandi, Bi Gitau aliwahimiza wafanyakazi wa serikali ya kitaifa kukopa pesa za kununua magari kutoka kwa hazina hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma.

“Tuko na zaidi ya Sh3.8 bilioni ambazo hazijatumika katika hazina ya magari zinazosubiri maafisa wa serikali ya kitaifa kuchukua. Kwa sasa ni maafisa 100 tu ambao wamenufaika na Sh180 milioni pekee,” alisema Gitau.

Bi Gitau alisema hazina hiyo ilianzishwa kusaidia kuimarisha utendakazi na kuwapatia motisha maafisa wa serikali ya kitaifa. Pia ilinuiwa kuokoa maafisa wa umma wasikejeliwe na umma.

“Kumiliki gari kama mtumishi wa umma ni alama ya hadhi. Pia inavutia na kudumisha maafisa kazini,” aliongeza.

Kamishna wa Kaunti ya Nandi, Bw Geoffrey Omoding, ambaye pia alihudhuria hafla hiyo aliwahimiza maafisa hao kuchukua mikopo hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma na kubadilisha mtazamo wa umma kuhusu watumishi wa umma.

“Hii ni nafasi muhimu kwa maafisa wetu kumiliki magari na hivyo kuimarisha motisha wao kazini,” alisema Omoding.

Baadhi ya mahitaji ya kupata mkopo huo ni kujaza fomu ya kuuomba, kitambulisho cha kitaifa, nakala za taarifa za mishahara zilizoidhinishwa za miezi mitatu ya hivi punde, ripoti ya ukaguzi wa thamani ya gari na nakala ya cheti cha umiliki wa gari.

Watumishi wa umma wa kati ya gredi A hadi U wanahitimu kupata mikopo ya kati ya Sh600,000 hadi Sh4 milioni mtawalia huku maafisa wa serikali wakiwemo maafisa wakuu watendaji wa mashirika ya serikali na mawaziri wakinufaika na mkopo wa kati ya Sh5 milioni na Sh10 milioni.

Afisa anayesimamia hazina hiyo huhifadhi cheti za kumiliki gari hadi mkopo utakapolipwa kikamilifu. Madiwani pia wanapata mikopo ya magari ambayo mwaka jana ilibadilishwa kuwa ruzuku.

You can share this post!

WANASIASA WALIPUA MLIMA

NMG yatenga siku ya matumizi ya Kiswahili mara moja kila...