Habari Mseto

Watumizi wa mafuta taa mijini sasa wageukia kuni kwa upishi

September 7th, 2018 2 min read

Na FAUSTINE NGILA

WAKAZI wengi mijini ambao awali walikuwa wanatumia mafuta taa kupikia sasa wamegeukia kuni baada ya bei ya bidhaa hiyo kupanda hadi kiwango wasichoweza kumudu.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa mafuta taa sasa yanauzwa kwa kati ya Sh97 na Sh100 jijini Nairobi, Mombasa, mijini Kisii, Nakuru na Embu huku bei ikigonga Sh102 kwa lita mjini Wote, Kaunti ya Makueni.

Wakazi wengi waliohojiwa walisema kwa sasa hawawezi kuhimili gharama hiyo ya juu kwa kuwa hawana uwezo ikizingatiwa pia wana bidhaa nyingine muhimu na ghali za kununua kama unga na sukari.

“Bei ya mafuta sasa imepanda zaidi na kuifanya kuwa bidhaa ya matajiri. Nikiwa na Sh100, nitanunua unga wa kupika au mafuta taa? Heri nitumie kuni ambazo ni rahisi kupata. Makaa nayo hayashikiki, bei imepanda zaidi baada ya marufuku ya ukataji miti,” akasema Winnie Akhwisinwa, mkazi wa mtaa wa Uthiru, Nairobi na mama wa watoto watatu.

Wakenya wa tabaka la chini wamesalia kuteseka zaidi kwani bei ya gesi ya kupikia ni ghali mno kwa mifuko yao. Lakini kwa wale wenye uwezo, wamegura matumizi ya mafuta taa na sasa wamenunua gesi ya kupikia.

Ni hali hii ambayo imesababisha mauzo ya mafuta taa kupungua kwa asilimia 50 kwenye vituo vya mafuta na mitungi ya gesi kupata wateja wapya.

“Awali kabla ya bei kupanda, nilikuwa ninauzia wateja takriban lita 1,000 za mafuta taa lakini sasa wamepungua hadi 550 kwa siku. Nilikuwa nauza mitungi 20 ya gesi kila siku mwezi uliopita lakini sasa ninauza 50,” akasema Silas Emukule ambaye ni mhudumu katika kituo cha mafuta cha Total katika barabara ya Waiyaki, jijini Nairobi.

Katika Kaunti ya Makueni hali ni ngumu zaidi vituoni ambako lita ya mafuta taa inauzwa kwa Sh102 na Sh130 kwa lita madukani.

Wafanyabiashara wamelazimika kuongeza bei ya mafuta taa kwa wateja wa rejareja ambao nao wamepungua wakihepa kupunjwa.

Sicily Karimi ambaye ni mama wa watoto wawili jijini Nairobi anakiri kuwa biashara ya mafuta taa inadidimia na kuathiri pakubwa mapato yake.

“Kwa sasa mafuta taa ninanunua kwa Sh97 na kuuza kwa Sh120 lakini ni vigumu kupata wateja. Awali biashara ilikuwa imenawiri lakini sasa mapato ya mafuta yameyeyuka,” anasema huku akiongeza kuwa baadhi ya waliokuwa wateja wake sasa wanaokota kuni kando ya barabara kwa matumizi ya jikoni.

Ingawa Mahakam Kuu ya Bungoma Alhamisi ilisitisha kwa muda agizo la kuongeza ushuru wa asilimia 16 kwa bidhaa za mafuta, hatua hiyo haijasaidia lolote kwani Wakenya wanazidi kuumia.

Vituo vingi vya mafuta ya petroli kote nchini vimekauka, madereva wa teksi, matatu, magari ya kibinasfi, malori na bodaboda wasijue la kufanya.

Lakini wakazi wa mitaa ya mabanda mijini wameathirika zaidi, kwani wamekuwa wakitumia mafuta taa kupikia na sasa wametamauka kwani kuni hatimaye zitaisha washindwe kupika vyakula.