Habari Mseto

Wauguzi katika kaunti saba nao wajiunga na wenzao wanaogoma

February 20th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAUGUZI katika kaunti zingine saba wamejiunga na mgomo wa kitaifa ambao umeingia wiki ya tatu sasa, huku kaunti kadha zikiamua kuajiri wauguzi kwa mkataba ili kukwepa migomo siku zijazo.

Wauguzi katika kaunti za Tana River, Narok, Nakuru, Siaya, Kakamega, Bomet na Busia walianza mgomo Jumatano baada ya makataa waliyotoa kwa serikali za kaunti zao kufikia kikomo.

Wenzao katika kaunti ya Uasin Gishu walitarajiwa kususia kazi kuanzia leo Jumanne.

Tayari wauguzi wa Pokot Magharibi, Kisumu, Kisii, Wajir, Taita Taveta, Trans-Nzoia, Homa Bay, Garissa, Samburu, na Marsabit wanaendelea na mgomo huo wa kitaifa ulioanza Jumatatu, Februari 04.

Wahudumu hao wa afya wameapa kutorudi kazini hadi matakwa yao yatimizwe, licha ya agizo la Rais Uhuru Kenyatta kuwaonya dhidi ya hatua hiyo.

Waziri mkuu wa zamani Raila Odinga akiwa mjini Busia Jumamosi pia aliwaomba wauguzi kurudi kazini kwa maslahi ya wagonjwa.

Wauguzi wanasisitiza Mkataba wa Malipo (CBA) baina yao na serikali kuu na za kaunti utekelezwe kikamilifu.

Mkataba huo uliotiwa saini Novemba 2017 na Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) unahusu marupurupu ya kazi ya ziada na sare.

Marupurupu ya kazi yalifaa kuongezwa kutoka Sh 20,000 hadi Sh30,000 kila mwezi katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2017.

Nayo marupurupu ya sare yalistahili kuongezwa kutoka Sh10,000 hadi Sh30,000 kila mwaka.

Serikali ya Kaunti ya Murang’a jana ilitangaza kuajiri wauguzi 100 kwa mkataba kama njia ya kukwepa migomo siku zijazo.

Wauguzi hao waliajiriwa chini ya mpango wa Tiba Mashinani; mkataba wao utadumu kwa miaka mitano.

Akizungumza kwenye hafla ya kutiwa saini kwa mikataba hiyo katika uwanja wa Uhura, Gavana Mwangi Wa Iria alisema mtindo huo unanuia kukomesha tabia ya “muungano wa wauguzi kushika mateka taifa ili kudai nyongeza ya mshahara.”

“Katika kaunti hii wauguzi wataajiriwa kwa mkataba ili yeyote akiukiuka anafutwa kazi na nafasi yake kujazwa mara moja!” alieleza na kushukuru wauguzi katika kaunti yake kwa kukosa kujiunga na mgomo wao wa kitaifa.

Gavana Iria aliongeza kuwa watajadiliana na wauguzi wengine 100 ili kuwaajiri katika wiki mbili zijazo.

Kaunti ya Kisumu pia iliajiri wauguzi kadha kwa mkataba kazi wiki jana hususan kusaidia katika idara zilizoathiriwa zaidi na mgomo. Idara hizo katika Hospitali ya Kaunti ya Kisumu ni thieta, wadi ya akina mama kujifungua, kliniki ya watoto na utoaji chanjo.

Kufikia Jumanne, wauguzi 137 wanachama wa KNUN walikuwa wamerejea kazini huku 686 wakiwa bado katika mgomo.

Wauguzi wengine ambao wamerejea kazini ni wale wa Kaunti ya Kisii waliositisha mgomo wao Jumatatu jioni.

Baadhi ya waliorejea kazini awali ni wa Elgeyo Marakwet, Nyeri, Kirinyaga na Embu.

Katika hospitali ya akina mama kujifungua ya Pumwani, Nairobi, wauguzi wote wanachama wa KNUN walirudi kazini huku wale ambao ni wanachama wa Muungano wa Wafanyakazi wa Kaunti (CWU) bado wamesusia kazi.

TAARIFA za Stephen Oduor, Jadson Gichana, Gaitano Pessa, Ndungu Gachane na Francis Mureithi.

Imekusanywa na Carolyne Agosa