Habari Mseto

Wauguzi Mandera waanza mgomo

August 2nd, 2020 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

Wauguzi wa Kaunti ya Mandera wameanza mgomo unaoshinika serikali ya Gavana Ali Roba iwapandishe cheo na kuwapa mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Bw Abdirahman Mohamed Haji ,mwanachama wa muungano wa wauguzi Mandera alisema kwamba kikundi cha kwanza cha wauguzi kilianza mgomo Ijumaa.

“Tulipeana notisi ya mgomo Juli 10 na itaisha Jumatano ambapo tunaanza mgomo lakini  wataalaamu washaanza mgomo,” alisema.

Hatua hiyo ya kwenda mgomo imepelekea wananchi wa Mandera kutafuta huduma za afya kutoka hospitali za kibinafsi.

Kulingana na Bw Haji, serikali ya Mandera imekuwa ikiwapa wauguzi ahadi za uwongo kila wanapoponeana notisi ya mgomo.

“Kuanzia mwaka 2013 hakuna muuguzi yeyote aliyepandishwa cheo kaunti ya Mandera,”alisema.

Mwaka 2013 wauguzi waliorithiwa kutoka serikali kuu walipandishwa vyeo, na wakati muungano wa wauguzi ulitosa notisi ya mgomo 2015 gavana Roba alihahidi kuwapandisha cheo.

“Hii haikufanyika kulingana na Bw Haji na wakandaa mgomo 2017 lakini ujanja huo huo ndio ulitumika wakarudi kazini.”