Habari Mseto

Wauguzi Nairobi waendelea kugoma

September 17th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HUKU Baraza la Magavana (CoG) likitangaza kusitishwa kwa huduma katika serikali zote za kaunti kuanzia Alhamisi, Septemba 17, 2020, wauguzi katika kaunti ya Nairobi wamekuwa wakigoma.

Kwa siku tatu mfululizo wahudumu hao wa afya wamekuwa wakisusia kazi na kuandamana nje ya jumba la City Hall wakiitisha nyongeza ya mishahara na kuimarisha kwa mazingira yao ya kikazi.

Huku wakiwa wamebeba mabango wahudumu hao ambao wanafanyakazi kazi katika hospitali mbalimbali jijini walimkashifu Afisa Mkuu wa Afya katika Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi Dkt Ouma Oluga kwa kutochukulia matakwa yao kwa uzito.

“Dkt Oluga anafaa kujiuzulu ikiwa hawezi kusikia kilio chetu. Kile tunaulinza ni nyongeza ya mishahara, marupurupu na kuboreshwa kwa mazingira ya kazi tulivyoahidiwa,” akasema Bw John Mutua, ambaye ni mweka hazina wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi Nchini (KNUN), tawi la Nairobi.

Dkt Oluga ambaye aliteuliwa kwa wadhifa huo, mnamo Machi 25, 2002, zamani alihudumu kama Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU).

Haya yanajiri wakati ambapo huduma za afya zikiwa mojawapo ya zile ambazo zitasitishwa kuanza Alhamisi Septemba 17, 2020, kufuatia agizo lililotolewa na mwenyekiti wa CoG Wycliffe Oparanya.

Gavana huyo wa Kakamega aliamuru wenzake 46 kuwapa wafanyakazi wote likizo ya majuma mawili kutokana na mvutano unaoendelea katika seneti kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti

Kulingana na agizo hilo wagonjwa wanaotaka huduma za malazi hawatashughulikiwa kwani ni huduma za wagonjwa kutibiwa na kwenda nyumbani pekee zitatolewa, japo kwa uchache.

“Serikali zote za kaunti zinashauriwa kutoa ilani kwa wafanyakazi kwamba watapewa likizo ya wiki mbili na huduma zote zisizo muhimu zitasitisha. Na hospitali zote hazitawapokea wagonjwa wa kulazwa. Ni huduma chache tu za wagonjwa kutibiwa na kwenda nyumba zitatolewa,” Bw Oparanya, akasema.

Mnamo Septemba 3, 2020 mwenyekiti huyo wa CoG alisema kwamba seneti imekwamisha shughuli katika serikali za kaunti kwa kufeli kuelewana kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato kwa kaunti ndiposa kaunti zisambaziwe sehemu ya mgao wao wa fedha Sh316.5 bilioni.

Gavana huyo alisema hatua ya Seneti kufeli kukubaliana kuhusu mfumo huo umechangia serikali za kaunti kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi, wakiwemo wahudumu wa afya.

“Kwa hivyo tunatoa onyo kwa seneti kwamba ombi la kuivunjilia mbali inaweza kuwasilishwa na mwananchi yeyote kupitia mahakama kuu kulingana na kipengele cha 258 cha Katiba,” akasema.