Habari Mseto

Wauguzi wafutilia mbali mgomo

December 10th, 2018 1 min read

Na BENSON AMADALA

WAUGUZI wamefutilia mbali mgomo wao uliokuwa umepangiwa kuanza usiku wa kuamkia Jumapili.

Notisi ya mgomo huo ulionuiwa kulalamikia kucheleweshwa kwa utekelezaji wa makubaliano ya pamoja ya malipo kati ya wauguzi na serikali sasa inasema mgomo huo utafanyika Februaru 4, 2019.

Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) kilisema hatua hii imechukuliwa ili kutoa muda zaidi kwa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) iagize serikali za kaunti kutekeleza marupurupu yaliyokuwa kwenye makubaliano ya pamoja.

Katibu Mkuu wa KNUN, Bw Seth Panyako, alisema wauguzi watasusia kazi Februari 4 mwaka ujao kama SRC itakosa kuarifu rasmi serikali za kaunti kulipa marupurupu mapya ya wauguzi na kutekeleza makubaliano yaliyowafanya kusitisha mgomo wa mwaka uliopita.

Uamuzi huu ulitangazwa baada ya mashauriano ya wanachama wa baraza kuu la kitaifa la chama hicho.

Akizungumza akiwa Kakamega, Bw Panyako alisema serikali nyingi za kaunti zimejumuisha marupurupu mapya ya wauguzi kwenye bajeti zao za 2018/2019 hivyo basi kuna matumaini kwamba wana nia ya kulipa.

“Tulichogundua ni kwamba SRC ndio kikwazo kwani haijaidhibisha serikali za kaunti kutoa malipo hayo kwa wauguzi. Kwa msingi huu, tunaagiza SRC iwasilishe taarifa mara moja kwa serikali za kaunti kuhusu utekelezaji wa marupurupu hayo ili kuzuia kutatizwa kwa shughuli za afya kwa umma,” akasema.

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa makubaliano ya pamoja, marupurupu ya wauguzi yaliongezwa kwa Sh3,000. Yanahitajika kupanda hadi Sh3,500 katika awamu ya pili na ya tatu ya utekelezaji wa maelewano hayo.

Naibu Katibu wa KNUN, Bw Maurice Opetu, alisema ikiwa SRC itakosa kuruhusu serikali za kaunti kutoa malipo hayo kabla Februari 4, 2019, wauguzi hawatakuwa na budi ila kugoma.