Habari Mseto

Wauguzi wamtaka Boinnet amtie mbaroni Mugo wa Wairimu

November 7th, 2018 1 min read

Na CAROLYNE AGOSA

CHAMA cha Wauguzi nchini (NNAK) Jumatano kimemtaka Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet kumtia kizuizini daktari bandia Mugo wa Wairimu ambaye amekuwa akiendeleza huduma zake hatari mtaani Kayole, Nairobi, licha ya kushtakiwa miaka mitatu iliyopita.

Mugo wa Wairimu ambaye jina lake rasmi ni James Mugo Ndichu alishtakiwa 2015 kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuendesha kliniki bila kibali mtaani Githurai, kutoa dawa kwa wagonjwa bila idhini na kuwabaka wagonjwa.

Hata hivyo, kesi hiyo ilisambaratika 2016 baada ya mashahidi na waathiriwa kukosa kuandikisha taarifa ambazo zingetumika kutoa ushahidi katika kesi hiyo, licha ya maafisa kuwasihi kujitokeza.

Jumanne maafisa wa kitengo cha Flying Squad walikuwa wakimsaka kufuatia makala ya upekuzi iliyopeperushwa na televisheni ya NTV Jumapili, iliyoonyesha uozo ambao mshukiwa amekuwa akiendeleza katika kliniki nyingine aliyofungua Kayole.

Makala hayo yanaonyesha jinsi Bw Mugo anaendesha visa vya kuavya mimba, anabugia pombe ndani ya kliniki, kuendesha huduma pasipo kufuata kanuni za matibabu, na kuwafyonza wagonjwa.

Mkuu wa Flying Squad mjini Nairobi Musa Yego alisema mshukiwa anasakwa ili kujibu madai dhidi yake kwamba amekuwa akiendesha kliniki za kuavya mimba kinyume na sheria.

“Tunamsaka Bw Wairimu na tunamuomba ajiwasilishe kwa polisi ili kuhojiwa,” Bw Yego alisema.

Mugo wa Wairimu alifuzu kwa digrii ya Sayansi katika Uuguzi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi 2000. Hata hivyo, hajasajiliwa kama daktarri na Bodi ya Madaktari na Madaktari wa Meno (KMPDB).

Chama cha wauguzi Jumanne kilisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka thabiti.

“Tunamkana kabisa mkora huyo; kamwe yeye si mwuguzi. Vitendo anavyovifanya ni vya kishetani. Ushahidi upo wa wazi hakuna lingine linalohitajika kumfunga jela.

“Leo (Jumanne) tutamuandikia barua Inspekta Jenerali ili tapeli huyo atakapofikishwa kortini atambuliwe kama mhalifu mwingine yeyote,” alieleza mwenyekiti wa NNAK Alfred Obengo katika kikao na wanahabari mjini Nairobi.