Habari Mseto

Wauguzi watishia kuhama baada ya wenzao kudungwa visu Mama Lucy

February 19th, 2019 1 min read

NA AGGREY OMBOKI

MUUNGANO wa Kitaifa wa Wauguzi Nchini(KNUN) tawi la Nairobi umetishia kuwaongoza wanachama wake kushiriki mgomo baada ya wauguzi wawili kudungwa visu Jumamosi usiku katika hospitali ya Mama Lucy.

Katibu wa KNUN tawi la Nairobi Ediah Muruli alilaani uvamizi huo na kuwalaumu maafisa wa usalama waliokuwa wakilinda hospitali hiyo kwa kutoroka na kukwepa kukabiliana na wavamizi hao kutokana na uoga.

“Tunataka hatua za haraka zichukuliwe kushughulikia suala hili ili wanachama wetu waweze kuhakikishiwa usalama wao la sivyo tutaandamana na kuacha kufanya kazi,”

“Inashangaza kwamba maafisa wa usalama waliojukumiwa kutoa ulinzi walikimbia wavamizi hao walipokuwa wakiwakimbiza wauguzi ndani ya hospitali hiyo. Iwapo hawawezi kuwalinda wagonjwa na wafanyakazi kwa nini wanaruhusiwa kutoa huduma za ulinzi,” akasema Bi Muruli.

Hata hivyo alifichua kwamba usimamizi wa hospitali ya Mama Lucy utaandaa mkutano na kampuni iliyopewa kandarasi ya kutoa huduma za ulinzi ili kupokea maelezo kamili kwa nini maafisa wake walitimka mbio kwa kasi na kutorokea usalama wao wakati wa tukio hilo.

“Tunataka kujua namna wavamizi hao walivyoingia ndani ya hospitali wakiwa wamejihami kwa visu vikali. Iwapo waliweza kuingia na kusababisha majeruhi basi hata siku zijazo wengine wanaweza kuingia na kufanya makuu,” akaongeza.

Kamanda wa polisi wa eneo hilo Kenneth Murungi akizungumzia kisa hicho alisema polisi tayari wamewanasa washukiwa 2 wanaoendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Soweto wakisubiri kufikishwa mahakamani.