Habari Mseto

Waumini wa kanisa la Methodist wajitenga na kanisa kuu

January 28th, 2019 2 min read

Na MOHAMED AHMED

WAUMINI wa Kanisa la Methodist katika eneo la Pwani wamejitenga na kanisa kuu licha ya agizo la mahakama lililokataza kutawazwa kwa viongozi wa mrengo uliojitenga.

Mahakama ilikuwa imekataza kutawazwa kwa viongozi wa tawi hilo la Pwani jana. Lakini viongozi hao walitawazwa mnamo Jumamosi wakiongozwa na Askofu Wellington Sanga ambaye alitangazwa kuwa ndiye atakuwa mkuu wa mrengo huo.

Maaskofu sita ambao watasimamia makanisa hayo katika kaunti sita za Pwani pia walitawazwa Jumamosi.

Kanisa kuu lilikuwa limeenda mahakamani kusimamisha sherehe hiyo iliyopangwa kuandaliwa jana, wakati ambapo sherehe nyingine iliandaliwa ya kuapishwa kwa Askofu wa Mombasa Joshua M’ikiao. Sherehe hiyo ya Mombasa ilihudhuriwa na mkuu wa kanisa hilo Joseph Ntombura ambaye alisema kuwa hatambui kutawazwa kwa wakuu wa mrengo uliojitenga.

Jana, maafisa wa usalama walikuwa wameshika doria nje ya kanisa la MCK la Ribe Thomas Wakefield Memorial eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi ili kuzuia sherehe ya waliojitenga kuandaliwa.

Hata hivyo walipata habari kutoka kwa Askofu Sanga wakati wa hotuba yake “rasmi” kama kiongozi mpya wa tawi hilo la Pwani kuwa shughuli hiyo ilifanyika Jumamosi.

“Walipeleka amri ya mahakama nyumbani kwangu wakisema kuwa kusiapishwe mtu Januari 27 na sisi hatutofanya hilo leo kwa sababu jana Jumamosi tulifanya sherehe zetu. Tulitengeza daraja letu na tukafikia malengo yetu,” akasema Askofu Sanga.

Alisema kuwa tawi hilo la Pwani sasa litakuwa ndilo linamiliki rasilimali zote zilizoko chini ya kanisa la kuu la Methodist eneo hilo.

Vile vile alisema kuwa pesa zote ambazo zitakuwa zinakusanywa kutoka kwa waumini wa kanisa eneo la Pwani zitaenda mahali pamoja na sio kwenye hazina ya kanisa kuu.

“Leo ninataka kusema kuwa kile ambacho sisi tumefanya sio kujitoa kwenye kanisa la MCK lakini tumetekeleza ugatuzi ili tuwe na tawi letu wenyewe. Kwa sababu hiyo, ninataka nieleweke vizuri kuwa ardhi zote zile ambazo zinamilikiwa na kanisa la Methodist na ziko hapa Pwani sasa zitakuwa chini yetu,” akasema Askofu Sanga na kuongeza kuwa karibuni wataanzisha mpango wa kumiliki ardhi hizo kisheria.

Alisema kuwa hatua hiyo ya kujitenga inalenga kunufaisha Wapwani kupitia rasilimali ziliziko kwenye eneo lao.

“Tunafahamu kuwa kwa muda sasa viongozi wengi wa kanisa hili humu nchini wamekuwa wakikadamizwa na ndiposa sisi waumini wa Pwani tumeamua kuwa tutakuwa mfano ili kusitisha unyanyasaji huu,” akasema.

Askofu Sanga alitangaza kuwa kwa sababu ya kuishi vizuri na waumini wa dini ya Kiislamu katika eneo la Pwani, mrengo wao unapinga mpango wa kuzuai wasichana wa Kiislamu kuvaa hijab.