Habari Mseto

Waumini wa Kavonokya wasema wanaogopa polisi kuliko corona

March 30th, 2020 2 min read

Na Waandishi Wetu

WAUMINI wa dhehebu la Kavonokya, Jumaapili walijipiga kifua kwamba hawaogopi virusi vya corona bali wanachoepuka tu ni kuzozana na polisi, wakati walipotawanywa walipokuwa wamekusanyika kwa ibada.

Polisi katika Kaunti ya Tharaka Nithi waliwatawanya mamia ya waumini wa dhehebu hilo, waliokuwa wamekusanyika kanisani kwa ibada ya Jumapili.

Hii ni licha ya serikali kupiga marufuku mikutano yoyote ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kisa hicho kilifanyika katika kijiji cha Irunduni, Kaunti Ndogo ya Tharaka Kaskazini. Watu hao walipatikana na polisi wa Kituo cha Polisi cha Makutano, waliokuwa wakipiga doria katika eneo hilo.

Akizungumza na wanahabari baada ya kutawanywa, kiongozi wa dhehebu hilo, Bw Gitonga M’Mpururu, alisema waliamua kusimamisha ibada hiyo ili kuepuka kuzozana na polisi lakini si kwa kuogopa virusi hivyo.

Bw Gitonga analiongoza dhehebu hilo katika kaunti za Tharaka-Nithi, Meru, Embu na Kitui.

“Tunafahamu kuhusu virusi hivyo ijapokuwa hatuviogopi kwani ni adhabu ya mwanadamu kutoka kwa Mungu. Inawalenga watu wenye dhambi,” akadai.

Hii ni licha ya kuwa, sayansi imethibitisha ugonjwa huo haubagui kwa msingi wowote ule.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, pasta na waumini wake walikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kitale, baada ya kupatikana wakiendeleza ibada kanisani kinyume na maagizo ya serikali.

Polisi walifahamishwa na wananchi kwamba Pasta Bernard Tali wa kanisa la Impact Healing Church alikuwa akiwaongoza watu 20 kwenye ibada.Akithibitisha kisa hicho, Naibu Kamishna wa Trans Nzoia, Bw Sheriff Abdi alisema kuwa watu hao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kitale wakisubiri kufikishwa mahakamani leo.

Katika kaunti iyo hiyo, polisi walimkamata Kasisi Anthony Wanyonyi wa Kanisa la KAG Sirende, katika eneo la Sinoko, akiwa amejifungia kanisani na watu 32 wakiendelea na ibada.

Kamanda wa polisi katika eneo hilo, Bw Ayub Gitonga alithibitisha kisa hicho, akisema kwamba watu wao wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Sibanga.

Mjini Nakuru, makanisa mengi yalibaki mahame, kwani hakuna ibada zilizokuwa zikiendelea.Makanisa mengi yalikuwa yamefungwa huku walinzi pekee wakionekana wakiyalinda.

Misikiti mingi ilibaki imefungwa kwani hata maombi ya alfajiri hayakusikika.Mojawapo ya makanisa yaliyokuwa kimya ni Kanisa Katoliki la St Joseph’s Workers katika mtaa wa Racetrack, ambalo huwa maarufu sana miongoni mwa waumini.

Katika Kaunti ya Makueni, washiriki kadhaa wa Kanisa Katoliki waliamua kutumia njia ya kipekee kuendesha ibada ya misa.

Kasisi Boniface Kioko, anayeongoza Misheni ya Kiongwani aliendesha misa hiyo kupitia kijiredio kidogo, huku washiriki wakifuatilia matangazo hayo majumbani mwao.

Kijiredio hicho kimetengenezwa kwa njia maalum, ambapo huwekwa katika mlingoti mrefu ulio katika kanisa hilo.

Katika Kaunti ya Nairobi, makanisa mengi yaliamua kutumia njia za mitandao kuwafikia waumini wake.Makanisa hayo yalitumia mitandao ya Facebook na YouTube kupeperusha ibada zao huku waumini wakifuatilia moja kwa moja kutoka majumbani mwao.

Kwa mfano, katika Kanisa la Christ Is The Answer Ministries (CITAM) Valley Road, jijini Nairobi, washiriki karibu 15,000 walifuatilia mahubiri yaliyotolewa na Askofu David Oginde kwa njia ya Facebook.

Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa washiriki wa makanisa ya All Saints Cathedral, Nairobi na Jesus Is The Winner Ministries kati ya mengine.

Ripoti za Alex Njeru, Osborn Manyengo, Francis Mureithi, Pius Maundu na Wanderi Kamau