Habari Mseto

Waumini waandamana kumtimua pasta ‘anayeanika’ siri za ndoa zao

January 22nd, 2024 2 min read

OSCAR KAKAI NA LABAAN SHABAAN

HALI ya Kisirani Kanisani ilishuhudiwa katika kanisa la Redeemed Gospel Church, Chepareria, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Siku ya ibada Jumapili, washirika walijitenga na shughuli za kanisa na kuandamana dhidi ya Mchungaji wao Timothy Siamoi.

Waumini hawa waliojawa na mori walisema mchungaji wao ameshindwa kuwachunga wanakondoo akiishia kuanika hata siri za ndoa zao hadharani.

Mintarafu hii, wanataka mchungaji huyu atimuliwe na waletewe pasta mwingine.

Soma pia Kanisa lenye historia ya vurugu kupiga msasa maaskofu

Halafu Kanisa lafungisha ndoa za pamoja kusaidia kupunguza tabia za ukora wa kimapenzi Teso Kaskazini

Kisha Kanisa msalabani: Mjadala wa mapadri kuoa waibuka tena Vatican

“Ukijaribu kupeleka malilio yako kwa pasta na mkewe wanaenda kutangaza. Huyu ni pasta wa aina gani? Umekuja na shida za ndoa kisha unazisikia sokoni,” alisema muumini wa muda mrefu Beth Kagia akiongeza kuwa pasta hudinda kuwasaidia ili wengine wasipange foleni kwake wakitafuta msaada.

Kelele za tarumbeta zilisikika pamoja na matusi baina makundi yaliyopingana kama kasisi huyo anafaa ama hafai.

Malango ya kanisa yalifungwa kwa minyororo na makufuli ya waumini wakitaka mchungaji wao akae mbali huku wakibeba mabango yenye maandishi, Timothy Must Go.

Kadhalika, waumini wanaomuunga Mchungaji Siamoi walitia makufuli yao malangoni.

Ilibidi polisi wafike kanisani humo kuhakikisha maandamano hayo hayana uharibifu.

Mizozo hii iliibuka mnamo 2017 pindi tu mwanzilishi wa kanisa hilo Dkt Charles Otipo alipohamia Amerika na kumwachia mchungaji wa sasa kuwa Kasisi Mkuu.

Sasa wanataka mchungaji wao aondolewe na pasta mwingine aingie baadhi wakidai hajahitimu kusimamia wanakondoo.

“Huyu si pasta, ni mwalimu. Anafaa atoke arudi darasani kufunza watoto kwa sababu kazi ya uchungaji umemshinda,” alilalama mshirika mmoja.

Maandamano haya yaliongozwa na Mzee wa Kanisa David Leleywa ambaye pia anataka mkubwa wake atimuliwe.

“Tunatangaza sasa kuwa Timothy anafaa aende. Hakuna haja ya uongozi ambao unaleta uhasama baina ya waumini na kuharibu jina la kanisa kwa jamii,” alinguruma Bw Leleywa akijibiwa na shangwe za washirika wenzake.

Wengi wao waliteta kuwa tangu mchungaji huyu achukue usukani, waumini wamepungua kwa asilimia 75.

“Hata kama itabidi tusiwe na kanisa la Redeemed, pasta anafaa anunue shamba jingine afungue kanisa lake,” alifoka Josphat Mwaka.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Mchungaji Timothy Siamoi alisema ilibidi atafute hifadhi katika Kituo cha Polisi cha Chepareria ambapo alirekodi taarifa.

“Kuna baadhi ya watu wanataka kunibandua na ninashangaa kwa nini wanapinga mafunzo yangu,” alisema Pasta Siamoi ambaye amesifu uongozi wake wa miaka mitano akipinga madai kuwa pia yeye amefunga kanisa.

Ili kutafuta mwafaka, kamati inayojumuisha wawakilishi kutoka pande zote mbili imeundwa lakini suitafahamu bado inaendelea.