Habari Mseto

Waumini waliohofia laana ya pasta warudi kanisani

September 17th, 2018 1 min read

Na NICHOLAS KOMU

WAUMINI wa Kanisa la Gituiga PCEA lililoko Othaya, Kaunti ya Nyeri, jana walirejelea ibada katika kanisa hilo baada ya kususia kwa mwezi mmoja, ambapo walikuwa wakihofia “laana” waliyodai iliwekwa na pasta wao.

Kulifanywa tambiko kanisani jana wakati pasta huyo, Bi Irene Wangari, alipoomba msamaha na kubatilisha matamshi yake ya awali ambayo yalikuwa yamechukuliwa kuwa ya laana.

Kwa wiki nne zilizopita, waumini walikuwa wakifanya ibada nje ya kanisa lililokuwa limefungwa kwa kuhofia kwamba wangekutwa na mikosi kutokana na kile walichodai ni laana kutoka kwa pasta wao.

“Wazee walisusia ibada yake alipowasili. Aliimba tu akaomba kisha akaosha mikono kwa kutumia maji yaliyokuwa kwenye chupa,” akasema Bi Anne Wandia, mmoja wa waumini.

Ilidaiwa alisema “amenawa mikono” kutoka kwa kanisa la Gituiga.

“Hakuna mtu aliyejua kile alichomaanisha lakini kwa hakika, matamshi yake hayakuwa ya kubariki waumini. Waumini waliamini kwamba ni laana na hawakutaka kukumbwa na mabaya ndiposa hakuna aliyetaka kuingia kanisani,” akasema Bi Wandia.

Kanisa hilo limekuwa likikumbwa na mizozo ya uongozi kati ya wazee na pasta.