Habari Mseto

Waumini wamkataa askofu mpya

February 19th, 2019 2 min read

Na STEPHEN ODUOR

HALI ya sintofahamu iliibuka katika kanisa la Kimethodisti mjini Hola, baada ya waumini wa kanisa hilo kumkataa askofu mkuu wa jimbo hilo.

Askofu Japheth Uruji alikuwa ametoka jijini Nairobi, huku akiwa ameandamana na makasisi kadhaa wa jimbo hilo kwa ibada ya jumla, pale alipopata waumini wamefunga kanisa na kwenda ibada kwingine.

Ilibidi ibada hiyo kusitishwa kwa muda huku wageni kutoka maeneo mengine katika kaunti wakibaki mdomo wazi, huku baadhi ya wenyeji wa kanisa hilo wakitishia kuzua fujo.

Kulingana na viongozi wa kanisa hilo, hawakuwa wanamtambua tena Askofu Uruji kama askofu wao, na hivyo ujio wake haukuwa umetarajiwa wala kukubaliwa.

Walisema kuwa askofu huyo alikuwa wa kikundi cha makanisa yajulikanayo kama SINGWAYA, kikundi ambacho walikuwa wamekiasi kitambo na kujiunga na makanisa yaliyo chini ya mkusanyiko mpya wa Pwani.

“Hawezi kuja hapa atulazimishe na ratiba yake ilhali sisi tuko na zetu, kwanza sisi tuna askofu wetu, yeye ni wa kule Meru,” alisema Bw Zacharia Jilo, mzee wa kanisa.

Bw Jilo alisema kuwa hapakuwa na nafasi ya kasisi huyo kanisani mle, na wala hakuwa na mamlaka ya kuhudumu mle pasi na ruhusa za wenyeji.

Viongozi hao pia walisema kuwa shirika la makanisa ya Methodist ilijawa na ubaguzi, na ufisadi tele, hivyo basi kulemaza juhudi za makanisa yaliyo pwani kuendelea kiuchumi.

Walisena kuwa walikuwa wakichanga hela chungu nzima na kuzituma Nairobi, ila hawakuwai pata mgao sawia na ule wapatao wenzao wa maeneo ya bara.

Pia, walisema kuwa shirika hilo lilikuwa limepiga mnada miradi yote katika jimbo la Pwani baada ya kusgindwa kulipa mikopo, na hivyo halikuweza kuaminika na raslimali za kanisa.

“Tulikuwa hapa na hospitali za kanisa, kwa bidii zetu, sasa hazipo tena, shule zimepigwa mnada, miradi ya pwani yote yafanyiwa biashara tunasalia maskini, hatutakubali,”alifoka vikali Bw Wayu Barisa, mzee wa kanisa.

Hata hivyo Askofu Japheth Uruji alipuzilia mbali madai ya viongozi hao, akisema kuwa upinzani huo ulikuwa ukisukumwa na baadhi ya viongozi wa kanisa waliokwisha furushwa katika kazi ya ukasisi na bodi ya kanisa, na hivyo walikuwa na machungu.

“Hii ni mbinu tu ya kuwapotosha waumini, wanajua walifanya makosa ya aibu na sheria za kanisa zikachukua mkondo wake, ila sasa wanawapotosha waumini tu, “alisema.

Pia, alisema kuwa tetesi za kuwepo kwa mgawanyiko katika kanisa hilo hazikuwa na msingi, huku akisisitiza kuwa Methodist ni kanisa moja,chini ya kiongozi moja na hakuna wengine zaidi ya wale wanaotambulika kisheria.

Hata hivyo ibada ilifanyika chini ya hema huku polisi wakilinda doria.

Ugomvi wa kanisa la methodist sasa wazidi kupanua mianya yake, huku bodi kuu tawala ikipeleka kesi kortini kupinga kundi lipya la viongozi wapya walioapishwa kuongoza makanisa ya methodist yaliyopo katika jimbo la Pwani.